LIGI Kuu nchini Uingereza kuendelea tena hii leo, ambapo klabu ya Manchester City itashuka dimbani kuwakabili Everton, huku Chelsea ikiwa nyumbani itapata wakati wa kujiuliza mbele ya Astorn Villa mara baada ya kupoteza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Arsenal. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Chelsea walipoteza mchezo huo kwa mabao 3-1 mbele ya Arsenal ambao hawakupata ushindi katika michezo saba iliyopita ya Ligi Kuu toka walivyowafunga Manchester United Novemba Mosi, 2020.
Mpaka sasa Ligi hiyo imeshachezwa michezo 15 kwa baadhi ya timu, huku Liverpool akiendelea kuwa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 32 licha ya kubanwa mbavu na West Brom kwenye mchezo wa jana, nafasi ya pili ikishikwa na Everton akiwa na pointi 29 na nafasi ya tatu wakiwa Leicester City wenye pointi 28.
Mchezo mwengine utakuwa ni Crystal Palace ambao watakuwa nyumbani kuwakabili Leicester City na siku ya kesho tarehe 29 Desemba, 2020, Arsenal watakuwa ugenini dhidi ya Brighton, huku Manchester United ikiwaalika Wolves.
Ligi hiyo itaendelea tena siku ya Jumatano tarehe 30 Desemba, 2020 kwa michezo miwili ambapo Tottenham baada ya kulazimishwa sare dhidi ya Wolves ya bao 1-1, wataialika Fulham na vinara wa Ligi hiyo ambao pia ni mabingwa watetezi klabu ya Liverpool watakuwa ugenini kuwakabili Newcastle United.
Leave a comment