June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chaumma mguu sawa kujiunga Ukawa

Spread the love

HASHIM Rungwe, Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), amesema chama hicho kipo mbioni kujiunga na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakati wowote kuanzia sasa, anaandika Charles William.

Rungwe ambaye pia alikuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chaumma katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, amesema kuwa hakuna mtu yoyote timamu anayeweza kubeza mafanikio ya muungano wa vyama vya Ukawa.

“Ukawa imeleta mafanikio makubwa sana kwa vyama vya upinzani, hakuna mtu aliye timamu anaweza kubeza hilo. Sisi kama Chaumma, tupo kwenye mchakato wa kuangalia namna ya kuunganisha nguvu na Ukawa,” amesema Rungwe.

Rungwe alikuwa akizungumza asubuhi ya leo katika kipindi cha Power Breakfast, ambacho hurushwa na kituo cha Clouds Fm. Pamoja na mambo mengine pia ameelezea namna alivyokuwa akimuombea kura mgombea Urais wa Chadema, aliyekuwa akiungwa mkono na vyama vya Ukawa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Licha ya mimi kugombea urais, lakini kila nilipopita katika mikutano yangu nilikuwa nikiwambia wananchi, kama wanaona mimi sifai kuwa rais wa nchi basi wamchague mgombea wa Ukawa, mimi nilikuwa nikipambana na Chama Cha Mapinduzi tu,” amesema.

Alipoulizwa, kwanini chama chake kiliamua kusimamisha mgombea ilihali kilikuwa na imani na mgombea urais wa Ukawa, Rungwe amesema Chaumma kilikuwa chama kipya kilichohitaji kujitambulisha kwa watanzania.

“Chama cha siasa hakiendeshwi kwa one man show (uamuzi wa mtu mmoja), bali kwa maamuzi ya vikao vya chama, kwa kuwa sisi tulikuwa bado chama kipya cha siasa tuliamua tusimamishe mgombea urais na kwakweli tumefanikiwa kujitambulisha,” amesema.

Msimamo wa Ukawa

Akizungumzia kuhusu Chaumma kujiunga na Ukawa Dk. Vincent Mashinji,         Katibu Mkuu wa Chadema ambaye pia ni katibu mwenza wa Ukawa, amesema milango ipo wazi kwa Chaumma na vyama vingine vya siasa hapa nchini.

Ukawa ni Muungano unaohusisha vyama vya siasa, kama chama chochote cha siasa kinataka kujiunga na sisi basi kinakaribishwa, jambo la muhimu ni kuwa chama hicho kikituma maombi yake vyama washirika tutakaa na kuangalia kanuni zetu na kukipokea,” amesema.

Kuhusu vigezo kwa chama cha siasa kujiunga na Ukawa, Dk. Mashinji amesema, “Ukawa yenyewe ni Muungano wa Katiba ya Wananchi, kwahiyo moja kati ya kigezo muhimu kwa chama kujiunga na sisi, ni chama hicho kuamini katika katiba ya Wananchi.

Imani kwamba tunahitaji kuunganisha nguvu kupambana na kila aina ya uonevu na ukandamizaji na kuipigania Katiba mpya inatosha kuungana na sisi. Tunamkaribisha sana Rungwe na chama chake na tupo tayari kupokea maombi yake,” amesema.

error: Content is protected !!