May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chanjo ya Covid-19 mbioni kuingia Tanzania, wananchi kuchanjwa bure

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imesema imekamilisha muongozo wa kuingiza na kutoa chanjo ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid-19)  na kwamba zitaingizwa nchini hivi karibuni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumapili, tarehe 4 Julai 2021 na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi,  akitoa tamko la Covid-19 na muongozo wa  shule, jijini Dodoma.

”Muongozo wa kuingiza na kutoa chanjo umekamilika na mtu atachomwa kwa hiari yake. Chanjo hizo zitatolewa bure kwa wananchi. Serikali haitaruhusu uingizwajI wa chanjo kiholera na kuwatoza wananchi fedha kwaajili ya chanjo,” amesema Prof. Makubi.

Aidha,  Prof.  Makubi amezitaka taasisi za umma, vyuo vikuu, shule na sehemu zenye mikusanyiko ya watu wengi, kuzingatia miongozo ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya Covid-19, ikiwemo watu kunawa mikono na kuvaa barakoa.

”Miongozo ni ile ile inatakiwa ifuatwe shuleni, vyuoni na taasisi mbalimbali za elimu na hospitalini, kuweka miundombinu inayowezesha kunawa mikono kwa maji tiririka pamoja na kuvaa barokoa muda wote,” amesema Prof. Makubi na kuongeza:

‘Kwenye ofisi zote za serikali tunashauri watu waende wakiwa wamevaa barakoa na kabla ya kuingia kwenye ofisi hizo na kufanya shughuli ni vyema wanawe mikono.”

Muongozo huo umetolewa siku kadhaa tangu Rais Samia Suluhu Hassan, awatahadharishe wananchi juu ya uwepo wa wimbi la tatu la maambukizi ya Covid-19 , akisema kwamba kuna ishara juu ya uwepo wa wimbi hilo nchini na kuwataka wachukue tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.

Akizungumza na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), mkoani Dar es Salaam, tarehe 25 Juni mwaka huu, Rais Samia amesema nchini kuna wagonjwa zaidi ya 100 wa Covid-19.

error: Content is protected !!