WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu, ameagiza kuchukuliwa hatua watumishi wawili wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Mwalimu Omary Kwesiga, Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi na Scolastica Kanje, Afisa Muuguzi Msaizidi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Ni baada ya watumishi hao, Mwalimu Kwesiga na Kanje ambaye anafanya kazi Hospitali ya Mkoa ya Arusha kufanya igizo kwenye shughuli ya chanjo ya corona, kinyume cha taratibu na kanuni za utoaji wa chanjo.
Kitendo hicho kimeleta sintofahamu kwa wananchi kuhusu zoezi la chanjo linaloendelea nchini nzima baada ya kuzinduliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Julai 2021, Ikulu ya Dar es Salaam.
Taarifa ya Nteghenjwa Hoseah, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tamisemi, aliyoitoa leo Ijumaa tarehe 6 Agosti 2021 imesema, Waziri Ummy “amemuagiza Katibu Mkuu Tamisemi kumsimamisha kazi Mwalimu Kwesiga na Scolastica apelekwe kwenye baraza la wauguzi na wakunga kwa hatua zaidi.”
Katika kipande cha video cha sekundi 37 kinachosambaa mitandaoni, kinaonyesha jinsi muuguzi huyo, Scolastica akijaribisha kuchoma chanjo ya corona Mwalimu Kwesiga huku kiuhalisi hakufanya hivyo.
Tayari Agnes Mtawa, Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, amemuagiza muunguzi wa mkoa wa Arusha ambaye ni msimamizi wa taaluma katika mkoa, kumsimamisha kazi miezi mitatu, Scolastica “kisha kutoa taarifa ya zoezi zima lililopelekea muuguzi huyo kufanya kitendo hicho.”
Agnes kupitia taarifa yake kwa umma amewaasa wauguzi na wakunga kuzingatia viapo kwa kutia huduma kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma ili kuepusha usumbufu kwa wananchi usiokuwa wa lazima.
Leave a comment