December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Change Tanzania wamtetea CAG

Spread the love

IDADI ya makundi yanayojitokeza kumtetea Profesa Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) dhidi ya azimilo la Bunge la Jamhuri la kumtenga, imeongezeka. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taasisi ya wanaharakati inayotetea haki za kiraia nchini – Change Tanzania,- imewasilisha wito wa kulitaka Bunge kuondoa azimio hilo kwa maslahi ya taifa.

Hivi karibuni, Bunge limeazimia kutofanya kazi na Prof. Assad kwa madai ya kulidhalilisha aliposema Bunge ni dhaifu, wakati wa mahojiano na Kituo cha Redio cha Umoja wa Mataifa, nchini Marekani.

Wito wa Change Tanzania ulioungwa mkono na maelfu ya wananchi kupitia kura za maoni mtandaoni ‘Petition,’ umewasilishwa bungeni leo tarehe 8 Aprili 2019 na Mbaraka Islam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya taasisi hiyo.

Taasisi hiyo inaungana tasisi ama jumuiya zingine zinazotaka, mvutano kati ya CAG na Bunge umalizwe kwa kuwa, haliwezi kufanya kazi bila CAG kwa mujibu wa Katiba ya Nchi.

Baada ya kuwasilisha wito huo, Islam amesema, wao kama Watanzania wametimiza wajibu wao wa kikatiba wa kulinda uwajibikaji na usimamizi wa serikali kama Katiba ilivyoainisha.

“Mahusiano ya Bunge na CAG yako kikatiba na si suala la mtu binafsi. Ripoti ya ukaguzi wa fedha za serikali ni lazima zitayarishwe na Prof. Assad, Bunge lazima lijadili baada ya kulipokea taarifa hiyo kutoka ofisi ya rais ndani ya siku saba,” amesema Islam.

Aidha, taasisi hiyo imetoa wito kwa wabunge wanaounga mkono wito huo, wasimamie ndani ya bunge kwa kuwasilisha ombi hilo.

“Katika mfumo wa kidemokrasia, tumefundishwa kuwa, serikali ni ya wananchi kwa ajili ya wananchi, hivyo wabunge waelewe kuwa, wananchi tunataka kuona uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma kama ilivyoainishwa katika Katiba yetu,” amesema Mratibu wa Kitaifa wa Change Tanzania, Mshabaha Hamza Mshabaha.

error: Content is protected !!