May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Changamoto sugu: Wananchi Njombe Mjini wamfungia kambi mbunge 

Deo Mwanyika, Mbunge Njombe Mjini (CCM).

Spread the love

 

BAADHI ya Wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini, wamelazimika kuweka kikao na Mbunge wao, Deo Mwanyika, kujadili namna ya kumaliza changamoto  sugu zinazowakabili jimboni humo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar Es Salaam…(endelea).

Kikao hicho cha mkakati kimefanyika leo Jumamosi tarehe 15 Mei 2021, jijini Dar es Salaam, baada ya Umoja wa Wananchi wa Jimbo hilo walioko mkoani hapa, kumuita Mwanyika ili wamueleze matatizo yao kwa ajili ya kuyawasilisha bungeni yapatiwe ufumbuzi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Mamongolo Family, Gabriel Mwajombe,  amesema licha ya jimbo hilo kuwa miongoni mwa majimbo yanayozalisha kwa wingi mazao yanayolisha nchi nzima, limetelekezwa hususan katika masuala ya mawasiliano ya barabara na simu.

“Tumeona tukusanyike hapa kuangazia fursa na changamoto katika jimbo letu,  mfano za miundombinu ya barabara na mawasiliano ya njia ya simu. Sekta ya afya, maji, nishati ya umeme na kadhalika. Hayo ni kwa kutaja kwa uchache,” amesema Mwajombe na kuongeza:

“Haya yote tunataraji tutabadilishana mawazo na mbunge wetu pamoja na madiwani, tutakubaliana nini kipaumbele chetu kama Kata ya Makowo na Njombe Mjini kwa ujumla, katika kumaliza changamoto hizo.”

Naye Diwani wa Makowo iliyoko jimboni humo, Honoratus Mgaya, amesema “changamoto zilizoko kwetu sana sana ni miundombinu, hakuna barabara inayopitika msimu wote,  wakati wa kipupwe usafiri unakuwa wa shida. Wakulima wanaolima parachichi na chai unakuta wanaingiza kipato kikubwa kwa Serikali, mwisho wa siku barabara zinachangamoto.”

“Huku kuna pesa  tukaona vizuri mbunge aje tutoe taarifa hizi,  watengeneze barabara sababu wananchi wanachangia mapato ya Serikali lakini barabara chafu.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye kikao baina yao na Mbunge wa Njombe Mjini

Kama Serikali inatambua hawa ni wananchi wake wanafanya shughuli za kimaendeleo, umeme hauna budi kufika katika maeneo yao,” amesema Mgaya.

Akijibu malalamiko hayo, Mwanyika amesema atashirikiana na wananchi wa Njombe Mjini, katika kuleta maendeleo ya jimbo hilo.

“Katika mpango kazi wangu naendelea kuamini kwamba, tunahitaji kushirikiana na Wananjombe walioko nyumbani na Dar es Salaam, kuleta maendeleo.Nimezisikia kero nyingi na ndizo  zilinisukuma kugombea, nataka kufanya mabadiliko katika jimbo letu la Njombe na vijiji vyetu vyote,” amesema Mwanyika.

Mwanyika amekiri kwamba jimbo hilo lina changamoto za muda mrefu.

“Ukilinganisha tulicho nacho Wananjombe na maendeleo yetu naona kama ni mbingu na ardhi, kwamba kuna nafasi kubwa sana imeachwa. Naamini Wanajombe tuna mengi zaidi ya kujifanyia wenyewe na Serikali yetu kutufanyia kama walivyofanya maeneo mengine. Serikali huwa inaangalia na eneo limefanyaje ndipo inasaidia, ukilala unapata mgawo mdogo, amesema Mwanyika.

Mwanasiasa huyo amesema katika uongozi wake, atawaamsha wananchi wa jimbo hilo, ili waongeze juhudi katika kujiletea maendeleo.

Vijijini kuna changamoto nyingi,  sisi wazalishaji wakubwa katika nchi tunalisha nchi, kwa nini nchi haitupi barabara tuilishe vizuri?. Kwa hiyo tuna hoja, nilipeleka hoja ya maji bungeni nikihoji inawezekanaje maji yakawa shida? Umeme mmeongelea hapa lakini inawezekanaje miaka 60 ya uhuru tunashahaulikaje? Kwa nini tumesahaulika au tumelala usingizi? Mimi nimekuja kuwaamsha,” amesema Mwanyika.

error: Content is protected !!