Wednesday , 21 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema yafukuza wabunge wanne, wengine 11 kikaangoni
Habari za SiasaTangulizi

Chadema yafukuza wabunge wanne, wengine 11 kikaangoni

Spread the love

WABUNGE wanne kati ya 15 ‘walioasi’ uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutohudhuria vikao vya Bunge ili kujiweka karantini kwa siku 14, wametimuliwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Uamuzi wa kuwatimua umetangazwa leo tarehe 11 Mei 2020 na John Mnyika, Katibu Mkuu wa chama hicho mbele ya waandishi wa habari, wakati akieleza maazimio ya Kamati Kuu iliyoketi kwa siku mbili (9-10).

Wabunge hao ni Wilfred Lwakatare (Bukoma Mjini), Anthony Komu (Moshi Vijijini), David Silinde (Momba) na Joseph Selasini (Rombo).

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa tarehe 1 Mei 2020, aliwatawa wabunge wa chama hicho kujiweka karantini ili kuangalia kama wameambukizwa virusi vya corona ama la!

“Licha ya kuwataka wabunge wa Chadema kutohudhuria bungeni, tunawasihi wabunge wengine wote wa vyama vingine kutafakari kama kweli ni salama kuendelea na vikao vya Bunge katika mazingira yaliyopo,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walikaidi maagizo hayo na kuamua kuhudhuria shughuli za Bunge linalojadili bajeti ya mwaka 2020/21 hali iliyowafanya kuingia matatizoni na chama chao.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mnyika ametoa maazimio sita yaliyofikiwa akisema wabunge hao wamefukuzwa kwa kuwa, wamekiuka maagizo ya chama sambamba na kutoa maneno ya kashfa, kejeli kwa chama na viongozi wakuu.

“Komu, Selasin pamoja na kuwa wamepoteza sifa ya uanachama wa Chadema, wameendelea kutoa kauli za kejeli, kashfa, hivyo chama kimeazimia kuwafukuza uanachama,” amesema Mnyika.

hata hivyo, kwa nyakati tofauti Komu na Selasini wamejitokeza hadharani kuzungumza na waandishi wa habari kueleza kuwa baada ya Bunge hili la 11 kumalizika watajiondoa Chadema na kujiunga na NCCR-Mageuzi.

Akiwazungumzia Silinde na Lwakatare, katibu mkuu huto amesema, “sio tu wamekiuka maagizo ya chama, bali pia wamekuwa wakijitokeza kwenye vyombo vya habari na kutoa maneno ya kashfa, kejeli dhidi ya maagizo ya chama na viongoi wa chama. Hivyo kamati kuu imewafuta uanachama.”

MwanaHALISI ONLINE lilipomtafuta Silinde kujua undani wa suala hilo anasema, “Sina la kusema kwa sasa naendelea kutafakari.”

Katika mchango wake bungeni wiki iliyopita, Silinde aliueleza umma kwamba, iwapo Chadema haitomdhamini kwenye uchaguzi mkuu ujao, anaweza kudhaminiwa na chama kingine na kurudi bungeni.

Mnyika amesema, Kamati Kuu ya Chadema imemuagiza kumwandikia barua Job Ndugai, Spika wa Bunge kumtaarifu maazimio ya chama hicho ya kuwafukuza uanachama wabunge hao.

Kuhusu Mariam Msabaha (Viti Maalum), ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, yeye amevuliwa nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho na kumtaka ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua zaidi.

“Kwa kuwa huyu ni mjumbe wa kamati kuu alitakiwa kuonesha mfano wa utekelezaji wa maagizo ya chama, kamati kuu imeamua kumvua nafasi zake zote za uongozi ndani ya chama na kubaki na nafasi ya ubunge na atatakiwa ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua,” amesema Mnyika.

Pia, kamati kuu ya chama hicho imewataka wabunge wengine waliokiuka agizo hilo pasina kuonesha kejeli kwa chama hicho, kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua.

Mariam Msabaha, Mbunge Viti Maalum Zanzibar kwa tiketi ya Chadema

“Kuhusu wabunge wengine ambao wamekwenda kinyume na makubaliano ya chama lakini hawajaonesha utovu wa nidhamu, wala kukikashifu na kukejeli chama, kamati imeazimia wajieleze kwa nini wasichukuliwe hatua zaidi kwa kukiuka maagizo ya chama,” amesema Mnyika.

Wabunge hao ni; Susan Maselle , Joyce Sokombi, Rose Kamili, Latifa Chande, Lucy Mlowe, Lucia Mlowe, Lucy Magereli na Dk Sware Semesi (wote Viti Maalumu).

Wengine ni; Willy Qambalo (Karatu), Peter Lijualikali (Kilombero) na Japhary Michael (Moshi Mjini).

Kamati Kuu pia imeagiza, wabunge waliotii agizo la chama, wametakiwa wamalize siku 14 walizoagizwa na kisha warejee bungeni kama hali itakuwa shwari.

“Kwa kadri hali itakavyokuwa juu ya ugonjwa wa corona, kama siku zikimalizika na kama hali ikiwa inatia matumaini, watarejea na kuendelea na majukumu yao,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Mwinyi ateua waziri wa uchumi na uwekezaji Zanzibar

Spread the loveRAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi,...

Habari za SiasaTangulizi

Mvua yakatisha mkutano wa Chadema Mbeya

Spread the loveMKUTANO wa hadhara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),...

Habari za Siasa

Sugu atumia maandamano ya Chadema kumfikishia ujumbe Spika Tulia

Spread the loveALIYEKUWA Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi “Sugu”, ametumia maandamano...

Habari za SiasaTangulizi

Sakata la DP World na bandari lafufuka upya

Spread the loveSAKATA la mkataba wa kiserikali kati ya Tanzania na Imarati...

error: Content is protected !!