WANACHAMA saba wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani Mara wamevuliwa uanachama huku watatu wakiwekwa chini ya uangalizi kwa muda wa mwaka mmoja, kwa tuhuma za usaliti. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa jana Jumatano tarehe 10 Machi 2021 na Lucas Ngoto, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mara, wakati anazungumza na wanahabari mkoani humo.
Wanachama hao waliofukuzwa Chadema ni, aliyekuwa Katibu wa Chadema Jimbo la Tarime Mjini, Peter Magwi, Jacob Kenyanga (Mwenyekiti Baraza la Wazee Chadema Wilaya ya Tarime) na Tecla Johannes.
Wengine ni, Sabato Amosi, Samwli Okendo, Paul Mwita na Isaya Mwita.
Waliopewa onyo na kuwekwa chini ya uangalizi ni, Steven Matiko. Richard Choge, Katibu wa Chadema Wilaya ya Butiama na Farajani Marwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), wilaya ya Butiama.
Ngoto alisema, wanachama hao wamefukuzwa Chadema, kwa tuhuma za usaliti kufuatia hatua yao kukaidi agizo la chama hicho la kutowatambua wabunge 19 wa viti maalumu, waliovuliwa uanachama.
Alisema wanachama hao, walikisaliti chama hicho kutokana na kuwaunga mkono wabunge hao kwa kuwasindikiza bungeni mjini Dodoma, hasa Ester Matiko, aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini kupitia Chadema.
Mbali na Matiko, wabunge viti maalumu wengine waliofukuzwa Chadema ni, Nusrat Hanje, Halima Mdee, Esther Bulaya, Agnesta Lambart, Hawa Mwaigfunga , Grace Tendega, Jesca Kishoa na Tunza Malapo.
Wengine ni, Cecilia Pareso, Asia Mwadin, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.
“Wengi katika kwenda Dodoma, wameupinga msimamo wa chama hadharani, sababu chama kupitia kamati kuu kimewavua uanachama waliokuwa wanachama wetu, kitendo cha wao kwenda kuwaunga mkono bungeni maana yake wameupinga ule msimamo wa chama hadharani na hilo ni kosa la kimaadili,” alisema Ngoto.
Ngoto alisema “kwa kukaidi na kwa sababu wanazozijua wao baadhi ya viongozi wa Jimbo la Tarime Mjini wameratibu zoezi hilo, na walienda safari hiyo pamoja na wanachama wetu na mwisho wake waliingia bungeni na wakatambulishwa kama wageni wa Matiko.”

Ngoto alidai kuwa, kabla ya wanachama hao kutenda kosa hilo, walipewa onyo la kutoshirikiana na wabunge hao.
“Mwanzoni mwa Januari 2021 tulianza kupata taarifa kwamba baadhi ya viongozi na wanachama Mara wanaratibu zoezi la wanachama wetu kwenda Dodoma, kuwasindikiza ambao wamefukuzwa siku ambayo wanahudhuria bungeni mara ya kwanza,
“Sisi kama baraza la uongozi mkoa tuliitisha kikao, tulikubaliana tuwape tahadhari na kuzuia wanaoratibu zoezi wasishiriki safari hiyo sababu itakuwa inakiuka miiko ya chama chetu,”alisema Ngoto.
Wabunge hao 19 wa viti maalumu walifukuzwa Chadema tarehe 27 Novemba 2020, kwa tuhuma za kukiuka maagizo ya chama hicho ya kutopeleka wawakilishi wake bungeni, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Wanachama hao walikuka maagizo hayo baada ya kukubali uteuzi wa ubunge viti maalumu, ambapo waliapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, tarehe 24 Novemba 2020.
Haya CCM wakaribisheni na vitita vya noti mpya mpya
Pole chadema kwa yote yanayo kukuta lakini. Kwanza usichukue hatua io