Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema yatilia shaka mazimio wadau wa siasa, yasema haijutii kutoshiriki
Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatilia shaka mazimio wadau wa siasa, yasema haijutii kutoshiriki

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakijutii kutoshiriki mkutano wa wadau wa siasa, kikidai baadhi ya maazimio yaliyotolewa na washiriki wake, hayajajibu changamoto zinazolalamikiwa, ikiwemo madai ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi, tarehe 18 Desemba 2021 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akitoa msimamo wa chama hicho, dhidi ya maazimio hayo takribani 80, yaliyotolewa katika mkutano huo, kwenda Serikalini.

“Kwa kuyaona haya, mimi baada ya kusikiliza hili la tume ya uchaguzi pekee, limenifanya dhamiri yangu na nafsi yangu isijutie uamuzi wetu wa kutokwenda kwenye mkutano huo uliofanyika Dodoma,” amedai Mnyika.

Akichambua mapendekezo ya wadau huo dhidi ya Tume ya Uchaguzi, Mnyika amedai kuwa, yana utata kwa kuwa hayajazungumzia kabisa juu ya mchakato wa upatikanaji wa tume huru.

“Ajenda ya tume huru na utata kwa nini hapa haipo, naomba nisome ambavyo tulinukuu, katika maneno yaliyoizungumzia tume huru, inasema hivi; yanayohusu tume ya uchaguzi yamepokelewa na yanayotakiwa kufanyiwa kazi yatafanyiwa kazi, kwa maana hiyo imeshindwa kukiri sasa hatuna tume huru ya uchaguzi tuanze mchakato wa kuiunda,” amedai Mnyika.

Mnyika amedai kuwa, maazimio hayo yanaashiria kwamba hakuna tatizo la kikatiba kuhusu muundo na mfumo wa uchaguzi huru, bali yalihimiza wadau wa vyama vya siasa kuamini vyombo vya utendaji.

“ Tunachoambiwa tuiamini tume, kwa hiyo tatizo kuaminiana. Tatizo ni watu tu, hakuna tatizo la kimuundo, kimfumo, kikatiba na sheria kuhusu uhuru wa tume na mfumo mzima wa usimamizi wa uchaguzi huru na haki, kwangu mimi nasema hakukupitishwa azimio la tume huru,” amedai Mnyika.

Kuhusu madai ya katiba mpya, Mnyika amedai maazimio hayo yanapendekeza mchakato huo uendelee kusubiri na kuwa katiba iliyopo ifanyiwe marekebisho katika maeneo yenye dosari.

“Ukitaka kujua dhamira ni kusubiri kwenye maazimio hayo hayo kuna azimio linasema, wakati katiba inayopendekezwa inasubiri badae, hii katiba iliyopo sasa ipitiwe maeneo machache, ifanyiwe marekebisho lakini hayo maeneo hayasemwi ni wapi,” amedai Mnyika.

Katibu Mkuu huyo wa Chadema amedai kuwa, maazimio hayo yanapendekeza katiba pendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba, ipitishwe baada ya kurekebishwa maeneo machache yatakayobainika kuwa na kasoro, badala ya rasimu ya katiba ya Jaji Mstaafu, Joseph Warioba, iliyobeba maoni ya wananchi nchi nzima.

“Katika hayo yote yanasema katiba mpya isubiri na ikishasubiri itakapofika huko ichukuliwe katiba inayopendekezwa, iliyopitishwa na Bunge Maalum eti iangaliwe maeneo machache yenye kasoro, halafu ndio iwe katiba ya wananchi,”

“maana yake ni kinyume na rasimu ya wananchi, kinyume na maoni ya wananchi mliokusanya nchi nzima kuhsu mchakato wa katiba,” amedai Mnyika.

Wakati huo huo, Mnyika amedai azimio lililopendekza Baraza la Vyama vya Siasa kuweka utaratibu wa vyama kuadhibiana vinapokiuka taratibu za kufanya mikutano ya hadhara, ni la mtego dhidi ya vyama hivyo.

Rodrick Lutembeka

“Ukisikilzia maneno kwamba mikutano ya hadhara ni haki na vyama vipewe hiyo haki, vianze kufanya mikutano, utaona mikutano ya hadhara inatia matumaini kwa maana ya kufungua ukurasa mpya,” amedai Mnyika.

Mwanasiasa huyo amedai “lakini azimio linalosema sasa uweke utaratibu wa baraza kutatua migogoro ya ndani ya vyama, uweke utaratibu wa vyama kuadhibiana vinapokiuka utaratibu wa mikutano ya hadhara, kinaitwa self regulation. Pale ni kengele ya hatari na nazungumza sio kwa nia mbaya bali kwa uhalisia.”

Amedai kuwa, utaratibu huo kama utapitishwa katika Sheria ya Vyama vya Siasa, unaweza tumika vibaya kwa baadhi ya vyama kuminya haki za vyama vingine.

“Hichi wanachokiita vyama kuadhibiana ili baraza la vyama likae, katibu mkuu wa Chadema amefanya mkutano ameikosoa Serikali chama kingine kinaandika maandiko kwa baraza huyu amekiuka haki yake ya kufanya mkutano halafu wanakaa watu wasiofanya mkutano kwa wingi wanaamua kutoa adhabu,” amedai Mnyika na kuongeza”

“Kwa sababu hiyo katibu mkuu apigwe marufuku kufanya mkutano wa hadhara mwaka, hiyo zuio la mikutano linahamishiwa na kuletwa katika mfumo mwingine. Mtego huu sisi wengine tunauona.”

Mapendekezo hayo ya wadau wa siasa yamewasilishwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Baraza la Vyama vya Siasa, kisha kitaundwa kikosi kazi kwa ajili ya kuyapitia na kuyapitisha ili kwenda katika mamlaka husika.

1 Comment

  • Asante ndugu mnyika ondoa shaka pasipo na shaka walio wakilisha ni mfano bora ktk ulimwengu wa kisiasa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!