May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yatangaza mchakato mrithi wa Halima Mdee

Halima Mdee, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha)

Spread the love

 

BARAZA la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), limetangaza mchakato wa kuwapata viongozi wake ngazi ya juu, ikiwemo ya mwenyekiti iliyokuwa ikishikiriwa na Halima James Mdee. Anaripoti Matilda Peter, Dar es Salaam … (endelea)

Mbali na nafasi ya Mdee, ambayo yenyewe atatafutwa kaimu mwenyekiti, zingine ni kaimu makamu mwenyekiti (Bara), katibu mkuu, naibu katibu mkuu, bara na Zanzibar na mwenezi wa baraza hilo.

Catherine Ruge, Mweka Hazina wa Bawacha, amesema fomu za kuwania nafasi hizo, zimeanza kutolewa leo Alhamisi tarehe 25 Februari ma mwisho wa kuzirejesha ni 3 Machi 2021, saa 10:00 jioni.

Ruge aliyekuwa mbunge wa viti maalum kupitia Chadema amesema, gharama za fomu hizo ambazo zinatolewa ofisi za chama hicho makao makuu, kanda na zile za Bawacha ni Sh. 50,000.

Bawacha imetangaza kuanza kwa mchakato huo, ikiwa zimepita siku 90, tangu Kamati Kuu ya Chadema, chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kuwafukuza Mdee na wenzake 18.

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa kwa tuhuma za kukisaliti na kwenda kinyume na katiba ya chama hicho kwa kujipeleka bungeni, kisha kuapishwa na Spika Job Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum, tarehe 24 Novemba 2020.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa ni wale waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko. Katibu Mkuu wa Bavicha, Nusrat Hanje. Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga. Naibu Katibu Mkuu Bawacha-Bara, Jesca Kishoa na Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambat.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Mtwara, Tunza Malapo, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao.Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Baada ya kufukuzwa, tarehe 1 Desemba 2020, Mdee na wenzake 18 wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, walisema hawana lengo la kuondoka ndani ya chama hicho na watabaki kama ‘wanachama wa hiari’ wakati mchakato wa kukara rufaa ukiendelea.

Mdee na wenzake, wamekwisha kukata rufaa kwa Baraza Kuu la chama hicho, kupinga uamuzi huo wa kamati wa kuwafukuza na haijajulikana kikao cha baraza hilo, kitaitishwa lini.

error: Content is protected !!