July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yataja vigezo uteuzi wagombea

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kushoto) akiteta jambo Katibu wake, Wilbroad Slaa

Spread the love

SIKU chache baada ya zoezi la kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi za ubunge na udiwani kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kukamilika katika majimbo yasiyo na wabunge sasa chama hicho kimetoa waraka mzito kuhusu namna ya kusimamia kikamilifu hatua zinazofuata kwa mujibu wa ‘katiba na kanuni za chama.’ Anaandika Deusdedit Kahangwa … (endelea).

Waraka huo namba tatu (3) wenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/CIR/15/48, umetolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, ukiwataka watendaji wote wa Chama kujitenga na rushwa na kujiepusha na matumizi mabaya ya madaraka wakati wote wa mchakato wa “kura ya maoni” katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Vigezo vya kuwapata wagombea Ubunge Jimbo katika Chadema

Dk Slaa amevitaja vigezo muhimu vitakavyotumiwa na Chadema kuwapata wagombea katika ngazi za ubunge na udiwani.

“Licha ya wagombea kuwa na sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi, Chama kitazingatia sifa” ambazo zimeainishwa katika Kanuni za Chama,” alifafanua Dk Slaa.

Kwa mujibu wa waraka huo, “sifa za kuzingatiwa katika kuteua wagombea katika uongozi wa Chama na Uwakilishi katika Vyombo vya Utawala” zimeainishwa katika Kanuni za Chama katika kifungu cha 7.6.

Dk. Slaa alizitaja sifa hizo kuwa ni pamoja na: uzoefu katika uongozi wa kisiasa ndani ya chama; mahusiano mazuri na viongozi wengine ndani ya chama; uadilifu katika uongozi wa nyuma kisiasa na kijamii; uwezo wa kutekeleza majukumu ya ngazi inayoombwa; uwezo wa kushirikisha na kushirikiana na watu wengine katika kutekeleza majukumu husika; ufahamu wa madhumuni, itikadi na falsafa ya Chama; uanachama hai katika msingi au tawi la chama katika eneo anamoishi au anakotoka mgombea; na ujuzi wa kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa wagombea wetu wanatimiza sifa hizo na nyinginezo kwa mujibu wa sheria za nchi zinazosimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani,” alisisitiza Dk Slaa.

Kwa upande wa wagombea ubunge, sifa “nyinginezo kwa mujibu wa sheria za nchi,” zinazoongelwa na Dk Slaa, zimetajwa katika ibara ya 67 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania (1977) ibara za 67(1) (a), 67(1) (b) na 67(2)(b), mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo ni raia wa Tanzania, ametimiza umri wa miaka ishirini na moja, anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza, ni mwanachama wa chama cha siasa,ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa, na anazo akili timamu.

Aidha, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania (1977) ibara ya 67(1)(c), mtu atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge ikiwa, katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi hajawahi kutiwa hatiani katika mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.

Aidha, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania (1977) ibara ya 67(2)(c), mtu atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge ikiwa mtu huyo hajawahi kuhukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu.

Vile vile, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania (1977) ibara ya 67(2)(d), mtu atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge ikiwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu mtu huyo hajapata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kuhusu wagombea wa Viti Maalum vya Ubunge na Udiwani, Dk Slaa alibainisha kuwa Baraza la wanawake Chadema (Bawacha) imeongeza sifa za vigezo vya ziada vyenye lengo la kuwapata wagombea wanaokubalika katika jamii.”

Vigezo vya kuwapata wagombea Ubunge Viti Maalum katika Chadema

Kwa mujibu wa Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Taifa, Grace Tendega, kuna vigezo vya ziada vitano vilivyopitishwa rasmi na baraza hilo.

Kigezo cha kwanza ni kiwango cha uwajibikaji wa mgombea katika utekelezaji wa majukumu ya uanachama kupitia baraza la wanawake. Kiwango hiki kitatamkwa katika “fomu za siri” zitakazo jazwa na viongozi wa Chama katika ngazi za Wilaya, Mkoa, Kanda na ya Kitaifa.

Kigezo cha pili ni umri wa mgombea ndani ya chama, ambapo mgawanyo wa pointi utakuwa kama ifuatavyo: umri wa mwaka 1 hadi 5 pointi 2, umri wa miaka 5 hadi 10 pointi 4, umri wa miaka 10 hadi 15 pointi 6, umri wa miaka 15 hadi 20 pointi 8, na umri wa miaka 20 hadi 25 pointi 10.

Kigezo cha tatu ni ngazi ya uongozi alio nao mgombea ndani ya chama, ambapo mgawanyo wa pointi utakuwa kama ifuatavyo: ngazi ya msingi au tawi pointi 2, ngazi ya kata pointi 4, ngazi ya wilaya au jimbo pointi 6, ngazi ya mkoa pointi 8, na ngazi ya taifa pointi 10.

Kigezo cha nne ni kiwango cha elimu ya mgombea, ambapo mgawanyo wa pointi utakuwa kama ifuatavyo: elimu ya darasa la saba pointi 2, elimu ya cheti pointi 4, elimu ya diploma pointi 6, elimu ya shahada ya kwanza pointi 8, na elimu ya uzamili au uzamivu pointi 10.

Na kigezo cha tano ni uzoefu wa uongozi katika taasisi mbalimbali, ambapo mgawanyo wa pointi utakuwa kama ifuatavyo: uongozi katika ngazi ya kijiji au mtaa pointi 2, uongozi katika ngazi ya kata au shehiya pointi 4, uongozi katika ngazi ya wilaya pointi 6, uongozi katika ngazi ya mkoa pointi 8, na uongozi katika ngazi ya kitaifa pointi 10.

Tendega aliliambia gazeti hili kuwa, vigezo hivi vilipitishwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya Bawacha Taifa kilichofanyika mjini Dodoma mnamo 06-07 Februari 2015.

Kwa mujibu wa Tendega, kikao hicho kiliamua kwamba, mwanachama wa Chadema atakuwa amepoteza fursa ya kuwa mgombea wa Ubunge Viti Maalum ikiwa anayo sifa yoyote kati ya sifa zifuatazo: amekuwa na mahusiano mabaya na viongozi, wanachama na jamii; amekuwa mkwepaji wa majukumu na wajibu wake kwa chama, baraza la wanawake na jamii; au amekuwa na mwenendo wa kutiliwa mashaka katika uaminifu wake kwa chama.

Pia, mwanachama wa Chadema atakuwa amepoteza fursa ya kuwa mgombea wa Ubunge Viti Maalum ikiwa amekuwa msaliti, mpika majungu na dhihaka kwa viongozi; amekuwa akishiriki siasa za makundi, majungu, fitina na ubaguzi dhidi ya jamii, viongozi na wanachama wenzake; au amekuwa akitoa au kupokea rushwa.

Marufuku dhidi ya rushwa

Mbali na kutaja vigezo vya uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali, waraka wa Dk Slaa umepiga marufuku “vitendo ambavyo vinakiuka Katiba na Kanuni za Chama wakati huu wa kuelekea kwenye zoezi la kura ya maoni.”

Dk Slaa amevitaja vitendo hivyo kuwa ni pamoja na “rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, makundi na upendeleo kwa baadhi ya wagombea, vitendo ambavyo vinafanywa na baadhi ya viongozi na wagombea wa nafasi mbalimbali za ubunge na udiwani.”

Vitendo hivyo ni pamoja na “kutoa fedha, vyakula, vinywaji, kusafirisha wajumbe kwa lengo la kuwahonga, kutoa au kushinikiza rushwa ya ngono, kutumia mamlaka ya kiongozi kupendelea upande mmojawapo na kuitisha vikao ambavyo sio halali kwa lengo la kukutana na wapiga kura.”

Hivyo, Dk Slaa amewataka viongozi wa chama, wanachama na wagombea wote kuusoma tena na kuzingatia kwa ukamilifu “Mwongozo wa Chama dhidi ya Rushwa toleo la mwaka 2012” katika wakati huu tunapoelekea kwenye zoezi la kura ya maoni ndani ya Chama.

Marufuku dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka

Matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Chadema ni jambo jingine lililopigwa marufuku kupitia waraka huu. “Ni kosa kwa mujibu wa katiba yetu kwa kiongozi kutumia madaraka yake kwa lengo la kujinufaisha yeye binafsi kinyume na kanuni na taratibu za Chama, ” alisema Dk Slaa.

Kwa mujibu wa Dk Slaa, wapo viongozi wa chama “ambao wanatumia hata vitendo vya ukabila, udini na ukanda katika kuwapendelea baadhi ya wagombea.” Lakini pia, alisema kuwa wapo viongozi wanaofanya “vitendo vya kuwachafua wagombea wengine kinyume kabisa na mwongozo wa kutangaza kusudio la kuwania nafasi za uongozi kwenye Chama, Mabaraza na Serikali vifungu vya 1(d), 1 (e) na 1 (f).”

Dk Slaa amekemea vikali tabia hii mbovu akitishia kuwachukulia hatua wote watakaothibitika kutumia vibaya madaraka yao.

error: Content is protected !!