August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yasisitiza ‘jino kwa jino’

Spread the love

SIKU Moja baada ya kuonywa na Msajili wa vyama vya siasa hapa nchini, Jaji Francis Mutungi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibuka na kusema, oparesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) ipo palepale, anaandika Pendo Omary.

Jaji Mutungi, katika taarifa yake kwa siku ya jana alisema, “Tamko la Chadema limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, linaloudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.” Alikuwa akizungumzia tamko la maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho.

Tamko lililotolewa na  Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema taifa aliyetangaza kuwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya chama hicho imeazimia kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano kote nchini kuanzia 1 Septemba ili kupinga udikteta unaomea hapa nchini.

Salum Mwalimu, Naibu Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar) amesisitiza hii leo jijini Dar es salaam kuwa maazimio ya chama hicho yapo pale pale na kwamba maandalizi ya msingi ya utekelezaji wake yameanza.

“Hatutarudi nyuma, hatutatishika, wala hatutatetereka. Kwa siku chache UKUTA huu umekuwa imara hata kabla ya siku hiyo ya 1 Septemba na tumepokea salamu kutoka kwa watu wa kada mbalimabali, taasisi na jumuiya mbalimbali wakitutia moyo juu ya jambo hili,” ameeleza.

Mwalimu amedai kuwa operesheni inayojulikana kama UKUTA ni mioyo ya watanzania wote na si chadema tu.

“Kufanya siasa ni wajibu wetu, siyo hisani ya mtu mmoja au kikundi cha watu. Ni wajibu wetu, ni haki yetu iliyo ndani ya sheria inayoongoza vyama vya siasa na kanuni zake,” amesema Mwalimu.

Tayari pia Rais John Magufuli amesikika mchana wa leo akiwa ziarani mkoani Singida akidai kuwa, “wanaotaka kuvuruga shughuli za maendeleo watakiona cha moto.”

 Kauli hiyo inaonekana kuilenga Chadema pamoja na mpango wake wa kuendesha maandamano na mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.
error: Content is protected !!