January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yashtukia hujuma BVR Dodoma

Msimamizi wa mashine za kuandikisha daftari la kudumu la wapiga kura (BVR) akimuandikisha mpiga kura

Msimamizi wa mashine za kuandikisha daftari la kudumu la wapiga kura (BVR) akimuandikisha mpiga kura

Spread the love

ZOEZI la uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR limeingia dosari katika Manispaa ya Dodoma, baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA),kudai kuhujumiwa na mmoja wa Afisa muandikishaji kukutwa usiku kituoni akiwa anawaandikisha watu. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Madai hayo yalitolewa mjini hapa jana na Mkurugenzi wa Oganezesheni na Mafunzo na Usimamizi wa Kanda, Benson Kigaila wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Kigaila amesema kuwa jana mnamo majira ya saa 2.5usiku walimkuta Afisa muandikishaji anayejulikana kwa jina la Helen Maungo katika kituo cha shule ya sekondari kiwanja cha ndege katika Kata ya Kiwanja cha ndege akiwaandikisha watu.

“Afisa huyo wa Tume awali alikuwa akiandikisha katika kituo cha shule ya msingi Mlimwa na baada ya hapo alifunga kituo kwa mujibu wa kanuni ya Tume ya uchaguzi saa12jioni ambapo alihama kituo na mashine za BVR na baadae saa2.5usiku tulimkuta kituo cha Kiwanja cha ndege baada ya kutuona mkurugenzi alikuja akampakia kwenye gari na kuondoka nae, hii ni hujuma,” amesema.

“Vijana wetu ambao ni mawakala walimkuta mama huyu peke yake kituoni akiwa na watu wamepanga foleni wanajiandikisha lakini tulipompigia simu Mkurugenzi hakuchukua hatua yeyote bali alimbeba kwenye gari na kuondoka nae,” amesema.

Aidha, Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa kosa hilo ni hujuma na inaonekana ni mbinu ya mkurugenzi wa manispaa ya Dodoma ili kuweza kuwaandikisha watu kinyemela ambao wanawataka wao.

Hata hivyo amesema kuwa kuanzia jana vijana wao wa ulinzi wa CHADEMA watazisindikiza mashine za BVR wajue zinalala wapi kwani hawataki hujuma wao wanasimamia sheria.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la wanawake Taifa (BAWACHA) kunti Majala alisema kuwa zoezi hilo limekuwa na changamoto hasa vijijini vijana ambao wana miaka 17 na miezi nane wamekuwa wakizuiwa kuandikishwa na mabalozi, watendaji wa vijiji na kata licha ya sheria ya uchaguzi kuruhusu.

“Nimeshuhudia mimi mwenyewe vijana hawa wakiwekwa ndani na polisi vijana wa Chemba ambao walitaka kujiandikisha,”amesema Majala.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Augustino Kalinga alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo alisema yupo kikaoni..

Nae Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma David Misime akizungumzia tukio hilo amesema kuwa hana taarifa kuhusiana na suala hilo lakini pia masuala hayo anayehusika ni Mkurugenzi wa Manispaa.

error: Content is protected !!