CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekosoa msimamo wa Baraza la Vyama vya Siasa wa kuipa muda Serikali katika mchakato wa marekebisho ya Katiba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Msimamo huo umetolewa leo tarehe 15 Septemba 2023 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akiwasilisha tamko la chama hicho kuhusu maadhimisho ya siku ya demokrasia duniani.
“Umma usikubaliane na maazimio ya mkutano wa baraza wa tarehe 13 Septemba 2023 ya kukwepa mahitaji ya haraka ya marekebisho ya Katiba ya 1977 katika Ibara zitakazowezwaha chaguzi huru na haki 2024 na 2025.
Aidha, usikubaliane na azimio la kuipa muda Serikali kuendelea kutathikini iwapo uchaguzi wa Serikali za mitaa uendelee kusimamiwa na TAMISEMI kupitia kanuni za Waziri au tume ya uchaguzi,” imesema taarifa ya Mnyika.
Mnyika amesema Serikali inatakiwa kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya Katiba ya 1977 kwenye mkutano ujao wa Bunge wa Oktoba 2023, kuwezesha chaguzi huru na haki, pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024 kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Kwa tafsiri nyepesi demokrasia ni mamlaka ya watu na uchaguzi ni mamlaka ya watu kuweka watu wa kuwaongoza. Hivyo itakuwa ni unafiki kijivunia uwepo wa demokrasia nchini ikiwa wananchi hawana nguvu na mamlaka ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa uhuru, haki na uadilifu,” Amesema Mnyika.
Katika hatua nyingine, Mnyika amewataka vijana kushiriki shughuli za demokrasia na siasa.
Leave a comment