Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema yanyang’anywa halmashauri Karatu
Habari za SiasaTangulizi

Chadema yanyang’anywa halmashauri Karatu

Bendera ya Chadema
Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tayari kimepoteza uongozi wa moja ya ngome yake kuu iliyokuwa inaishikilia kwa takribani miaka 25 mfululizo. Ni halmashauri ya wilaya ya Karatu, mkoani Manyara. Anaripoti Mwandishi Wetu AidanAziz kutoka Arusha … (endelea).

Habari kutoka mjini humo zinasema, tayari mwenyekiti wa halmashauri hiyo ameng’olewa kwenye nafasi yake, baada ya mmoja wa madiwani wa chama hicho, Sophia Shauri, kukisaliti chama chake.

Sophia, ambaye ni diwani wa Viti Maalum, aliungana na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kusaini “waraka wa mashitaka dhidi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jubleti Mnyenye.”

MwanaHALISI ONLINE limeelezwa kuwa katika kufikia hatua hiyo, diwani huyo alikuwa ameshawishiwa na na baadhi ya viongozi wa CCM kuwa ikiwa ataridhia kusaini mashitaka hayo, atalipwa ujira na kulindwa udiwani wake.

Mkutano wa Baraza Maalum la Madiwani ulioitishwa leo, tarehe 2 Septemba 2019 na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Waziri Moris, ndio umehitimisha uongozi wa miaka 25 wa Chadema katika halmashauri hiyo.

“Leo tumenyang’anywa halmashauri yetu ya Karatu tuliyoipigania kwa jasho na damu kwa takribani miaka 25. Hili ni jambo la kusikitisha sana. Tumenyang’anywa halmashauri hii, kutokana na ubinafsi wa baadhi ya viongozi wetu, waliotanguliza maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya chama,” ameeleza mmoja wa viongozi chama hicho wilayani Karatu kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Amesema, “lakini namshukuru Mungu sana, nimekitumikia chama changu kwa uadilifu mkubwa. Hakika, nimekitendea haki. Nimepigana na nimeshinda majaribu yote dhidi yangu.”

Amesema, kinachoiponza Chadema, ni ubinafsi wa baadhi ya viongozi wake, hasa katika suala la kushughulikia migogoro na kulindana, huku baadhi ya watu wanaotajwa kuwa hawana watetezi kwenye ngazi ya juu, wakitolewa kafara.

Kupatikana kwa taarifa hizi, kumekuja mwaka mmoja tangu MwanaHALISI Online liripoti kuwa “ngome pekee ya Chadema liyokuwa imesalia – halmashauri ya wilaya ya Karatu – iko hatarini kuvunjika.”

Mwandishi wa MwanaHALISI aliyenukuu baadhi ya vyanzo vya taarifa alieleza kuwa Chadema kiko hatarini kupoteza halmashauri hiyo, kufuatia kuibuka kwa mgogoro mkubwa wa uongozi ndani ya wilaya hiyo.

Mgogoro uliosambaratisha chama hicho, unadaiwa kuwa ulichochewa na mmoja wa viongozi wandamizi wa Chadema wilayani Karatu (jina tunalo), wakati wa kinyang’anyiro cha kumsaka makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Septemba mwaka jana.

Habari zinasema, hofu ya kiongozi huyo inayotokana na kutaka kuendelea kumiliki nafasi yake, kulimfanya kukusanya baadhi ya madiwani, wakiwamo wa Viti Maalum na kuwashawishi kwa njia ya mlungula, ili anayeamini kuwa “hasimu wake” kisiasa asiweze kupenya.

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa anagombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa halmashauri, ni Sabina Marmo, diwani wa Viti Maalum na katibu wa madiwani, kanda ya Kaskazini.

“Hatua ile ikawafanya baadhi ya madiwani wetu, akiwamo Yotham Manda, aliyekuwa diwani wa kata ya Qurus na Ally Bytoo, aliyekuwa diwani wa kata ya Endamaghan, kujiuzulu nyadhifa zao kwenye chama na kutimikia CCM. Huo ukawa ndio mwanzo wa hama hama ya madiwani na hatimaye leo, tumenyang’anywa rasmi halmashauri yetu,” ameeleza kiongozi mwingine wa Chadema katika wilaya hiyo.

Kigogo huyo aliagiza madiwani watatu wa Viti Maalum, Sophia Shauri, Cristine Safari na Levina Emmanuel, kutomchagua Sabina kwa madai kuwa nitishio kwa harakati zake.” Sophia aliyetumiwa wakati huo, ndiye huyo huyo aliyegeuka Yuda.

Yotham alikuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo. Katika uchaguzi huo, aliamua kujiondoa na kumuunga mkono Sabina. 

Aidha, MwanaHALISI liliripoti kuwa madiwani wengine wanne wa kata, walikuwa mbioni kuondoka ndani ya chama hicho, kabla ya Oktoba mwaka huu. Ndivyo ilivyotokea. 

Kama hiyo haitoshi, Sabina ambaye alijitosa katika kinyang’anyiro hicho, ghafla alisukumiziwa zengwe la tuhuma za kuuza madiwani, kusaliti chama na kushirikiana na viongozi wa CCM, ili kuhalalisha mpango haramu wa kumfukuza uwanachama wa chama chake.

Aliyeongoza mkakati huo, alikuwa mwenyekiti wa wilaya wa Chadema wilayani humo, Joseph Selestin Lolo, anayedaiwa kuwa alikuwa anatumiwa na CCM kuingiza mgogoro ndani ya chama hicho.

“Yule kigogo wa ndani ya Chadema, hakujua kuwa Lolo alikuwa anatumika na CCM. Alidhani anamsaidia yeye kupambana na mbaya wake. Kumbe haikuwa hivyo, aliuchukua mgogoro huo kuinufaisha CCM,” ameeleza kada mmoja wa Chadema wilayani humo.

Mtoa taarifa wetu anasema, tayari mwenyekiti huyo wa wilaya ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Mazingira Bora, ametimkia CCM, huku Sabina aliyekuwa anatuhumiwa kuuza madiwani na kupachikwa majina mabaya, akiendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa chama hicho.

Madiwani wengine waliondoka ambao walikuwa upande wa kigogo huyo, ni Lazaro Bajuta. Yeye aliahidiwa iwapo watatoa kura kwa mshindani wa Sabina, atazawadiwa ujumbe wa Kamati ya Fedha.

Wengine waliondoka na kufanya halmashauri kuchukuliwa na CCM, ni pamoja na Benedictor Mwodaha, Josephat Martin na John Zakaria. 

Aliyepata kuhudumu kwenye nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri ya Karatu kwa vipindi vitatu mfululizo, Lazaro Massay, ameeleza MwanaHALISI ONLINE kuwa sababu ya Chadema kupoteza halmashauri ya Karatu, ni ubinafsi wa baadhi ya viongozi, wakiwamo madiwani.

Anasema: “Nimewahi kumueleza mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuwa hapa kuna tatizo ambalo linahitaji utatuzi wa haraka. Nimeeleza haya wakati nikiwa mjumbe wa Kamati Kuu, nimeeleza hayo nikiwa mwanachama wa kawaida. Lakini  hakuna aliyenisikiliza.” 

Anasema, “niliwaambia kabla ya mambo hayajaharibika, wachukue hatua. Vinginevyo, hiki chama kitazikwa hapa Karatu.“

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kasekenya aipa Tanroads wiki kukarabati barabara Morogoro

Spread the loveNaibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wiki moja...

Habari za SiasaTangulizi

‘Aliyemtonya’ Lissu kuhusu rushwa arejea madarakani

Spread the loveMwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Tutaendelea kupigania malengo ya afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Tanzania...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NHC yadai bil. 2.1 taasisi za Serikali, Waziri atoa maagizo

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii...

error: Content is protected !!