August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yanena kuhusu Ukuta Oktoba 1

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa ufafanuzi juu ya hatma ya kuzinduliwa kwa Operesheni Ukuta na kusema bado hakijapokea mrejesho kutoka kwa viongozi wa dini mpaka sasa, anaandika Charles William.

Operesheni Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ilitangazwa na Chadema tarehe 27 Julai mwaka huu, kuwa ingezinduliwa Septemba mosi mwaka huu na kuibua mvutano mkali baina ya Chadema na Jeshi la Polisi kabla ya kuahirishwa mpaka Oktoba mosi mwaka huu.

“Tunatangaza kuahirisha mikutano na maandamano ya Ukuta kwa kuwa viongozi wa dini wametuomba tuwape angalau wiki tatu ili wafanye mazungumzo na Rais John Magufuli ili kutafuta suluhu ya suala hili na kama ikishindikana basi tutaifanya Oktoba mosi mwaka huu,” alisema Freeman Mbowe Agosti 31, mwaka huu.

Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema taifa na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni.

Akijibu swali la mwandishi wa MwanaHALISI online juu ya yalipofikia mazungumzo ya viongozi wa dini na Rais Magufuli pamoja na hatima ya kufanyika kwa operesheni Ukuta, Salum Mwalimu, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema amesema;

“Kama kuna vyombo vya habari vinaripoti kuwa Rais Magufuli amekataa kuonana na viongozi wa dini, hilo hatuwezi kulisemea kwasababu bado hatujapata mrejesho kutoka kwa viongozi wa dini.”

Alipoulizwa kuhusu muda wa siku tano uliobaki kabla ya tarehe ya kufanyika kwa uzinduzi wa operesheni hiyo, Mwalimu amejibu kuwa, “Ukuta si tarehe. Ukuta ni fikra zinazoishi ndani ya mioyo ya watu na zitaendelea kuishi. Suala siyo kubaki kwa siku tano au kumi.

Tunasubiri tupate mrejesho kutoka kwa viongozi wa dini halafu tutafanya uamuzi juu ya suala hilo.”

Jumatano ya wiki hii, gazeti moja la kila siku liliripoti kuwa Rais Magufuli amekataa kuonana na viongozi wa dini. Hata hivyo gazeti hilo lilidai kuwa Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu amesema viongozi hao watapangiwa tarehe ya kuonana na rais.

Habari ya gazeti hilo iliyokuwa na kichwa cha habari, “Rais Magufuli awatosa viongozi wa dini.” ilidai kuwa mpaka Jumanne wiki hii, barua ya viongozi hao wa dini hapa nchini ya kuomba kuonana na rais ilikuwa haijajibiwa.

error: Content is protected !!