June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yamvaa Kikwete

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Chadema, Bw. Arcardo Ntagazwa

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kuwa Rais Jakaya Kikwete, amepatwa kigugumizi kushughulikia watuhumiwa wakuu wa ufisadi katika Akaunti ya Escrow kwa kuwa yeye ni sehemu ya wizi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mchana, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Bw. Arcardo Ntagazwa amesema, “Rais Kikwete ni mmoja wa wanufaikaji wakubwa katika sakata hili.”

Alisema, “Kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kuchukua hatua madhubuti katika jambo hili, ni ushahidi wa wazi kuwa kigugumizi ambacho kimekuwa kikimkabili kinasukumwa na jambo kubwa nyuma yake, ikiwamo kujilinda binafsi na kulinda familia yake.”

 Akiongea kwa kujiamini, Ntagazwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho amesema, “Watanzania bado wanakumbuka kauli iliyotolewa bungeni wakati wa mkutano uliopita kuwa familia ya Rais Kikwete nayo iko nyuma ya sakata hili ikiwa mnufaikaji mkubwa kupitia kwa mtu aitwaye Albert Marwa ambaye ana uhusiano na familia hiyo.”

Amesema, Chadema ambacho kimekuwa kimbilio la wanyonge na tegemeo la wananchi, katika kulinda rasimaliza za taifa, ikiwamo fedha na kusimamia misingi ya uwajibijkaji, hakiwezi kunyamazia wizi wa aina hiyo.

Naye Benson Kigaila, mkurugenzi wa mikakati na kampeni akizungumza katika mkutano huo alimtaka Rais Kikwete kutumia hotuba yake ya kesho, kuwajibisha Prof. Muhongo, waziri wa nishati na madini; katibu mkuu katika wizara hiyo, Eliakim Maswi na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu.

Wengine ambao chama hicho kimesema wanapaswa kuondolewa katika nyadhifa zao, ni Silviacius Likwelile, katibu mkuu wizara ya fedha; Saada Mkuya, waziri katika wizara hiyo; Jaji Fredrick Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felicesmi Mramba.

Amesema, suala la miamala iliyofanyika kupitia Benki ya Stanbic, ikiwa ni sehemu ya kashfa hiyo, si suala la kufanyia mzaha au kupuuzwa hata kidogo.

“Ni kupitia benki hiyo ndiko kiwango kikubwa cha fedha zaidi ya Sh. 160 bilioni, zilibebwa kwa magunia, malumbesa na sandarusi ndani ya siku moja mchana kweupe, tena tunaambiwa wengine walikwenda kwa magari yenye nambari za serikali na fedha hizo zilipelekwa Ikulu ambako Rais Kikwete anafanyia kazi na kuishi,” amesisitiza Kigaila.

Amesema, “Ni ukweli ulio wazi kuwa hakuna benki ndani ya nchi yetu inayoweza kufanya miamala ya mabilioni ya fedha kwa kiwango hicho, bila BoT kuidhinisha. Kwa mantiki hiyo hiyo, Gavana Prof. Ndulu hawezi kukwepa uwajibikaji kwenye jambo hili zito kwa kuwa alilifahamu na kulilidhia.”

Tunatarajia Rais Kikwete ataueleza umma wa Watanzania hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi hawa wa umma na siyo kuja na visingizio vya miamala iliyochukuliwa katika Benki ya Mkombozi.

error: Content is protected !!