January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yambwaga Zitto mahakamani

Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini

Spread the love

SAFARI ya mapambano kati ya Zitto Kabwe-Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imefika ukiongoni baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali kesi yake namba 1 ya mwaka 2014, ya kuzuia asijadiliwe. Wanaandika Deusdedit Kahangwa na Sarafina Lidwino(endelea).

Uamuzi huo wa mahakama, unamweka Zitto njia panda ndani ya Chadema kutokana na Katiba yao kuzuia wanachama wake kuchukua hatua aliyopitia  badala ya kutumia ngazi za chama; Sasa chama kiko huru kuchukua uamuzi wowote dhidhi yake kuanzia leo.

Kanuni za kusimamia shughuli, mwenendo na maadili ya wabunge wa Chadema (2006), kifungu cha 8.0 (a) (x); zinasomeka ifuatavyo; “Chadema itashughulikia matatizo ya viongozi na wanachama kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa katiba ya chama, wala hata siku moja haitashughulikia mambo kama hayo mahakamani. Mwanachama atakayeshindwa kufuata taratibu na ngazi za chama hatavumiliwa na atafukuzwa uanachama”.

Katika hukumu yake leo asubuhi, Jaji Richard Mziray amekubaliana na hoja za Chadema zilizowasilishwa na mawakili wake, wakiomba kesi hiyo ifutwe kwa madai inakiuka katiba ya chama.

Kwa mujibu wa wakili wa Chadema, Peter Kibatala, katika hukumu yake Jaji Mziray amekubaliana na hoja hizo mbili na kumtaka Zitto kukilipa chama chake gharama zote za kuendesha kesi hiyo.

“Kadiri madai haya mawili yanavyohusika, Jaji Mziray amekubaliana na mawakili wa Chadema kuhusu madai kwamba kesi iliyofunguliwa na Zitto Kabwe ilikuwa imefunguliwa kinyume cha utaratibu wa kisheria,” amesema Kibatala.

Wakili Kibatala hakusema lolote kuhusu msimamo wa Jaji Mziray dhidi ya hoja nyingine tatu walizowasilisha Mahakama Kuu. Nakala ya hukumu ya leo haikuweza kupatikana mara moja ili kutoa picha kamili ya maamuzi husika.

Katika kesi hiyo, Zitto kupitia kwa mwanasheria wake, Arbert Msendo alifungua malalamiko dhidi ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa pamoja na Bodi ya Wadhamini.

Mapema mwaka jana, Zitto Kabwe aliitwa na Kamati Kuuya Chadema akitakiwa kujibu tuhuma za usaliti dhidi ya chama lakini hakuitikia wito huo.

Badala yake, alifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, akiiomba itoe amri ya kuzuia vikao vya Kamati Kuu ya Chadema kutojadili uanachama wake mpaka hapo kikao cha Baraza Kuu la Chadema kuitishwa, kupokea na kujadili na kuamua rufaa yake.

Katika rufaa yake, Zitto alikuwa anapinga uamuzi wa Chadema kumvua cheo chake cha Unaibu Katibu Mkuu.

Mnamo 21 Februari 2014, Mahakama Kuu kupitia hukumu ya Jaji John Utamwa, ilitoa zuio kwa Kamati Kuu ya Chadema kujadili na kuamua suala lolote linalomhusu Zitto.

Katika hukumu yake, Jaji Utamwa alidai kwamba, “itakuwa ni haramu kumtia hatiani mlalamikaji kwanza na kisha kumsikiliza baadaye.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili wa Chadema waliomba mapitio ya hukumu na leo maombi yao yamezaa matunda.

Awali, Wakili wa Zitto, alijibu kupinga uhalali wa maombi haya. Na baadaye, mawakili wa Chadema, Tundu Lissu na Peter Kibatala, waliwasilisha majibu yao.

Katika majibu yao ya 08 Agosti 2014 na 09 Oktoba 2014, mawakili Lissu na Kibatala, waliibua hoja tano kupinga mashitaka yaliyofunguliwa na Zitto dhidi ya uongozi wa Chadema.

Katika hoja ya kwanza, Lissu na Kibatala walidai kwamba, mashitaka ya Zitto dhidi ya uongozi wa Chadema yalikuwa ni batili kisheria kwa kuwa, yamekiuka kifungu cha 13 cha Sheria ya Kanuni ya Mwenendo wa Kesi za Madai, Sura ya 33, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.

Kwa maoni yao, Zitto alipaswa kusajili kesi yake katika Mahakama ya Wilaya na sio Mahakama Kuu, kama alivyofanya.  

Na katika hoja ya pili, walidai kwamba, mashitaka ya Zitto dhidi ya uongozi wa Chadema yalikuwa ni batili kisheria kwa kuwa, yamekiuka kifungu cha 7(1) cha Kanuni za Masjala ya Mahakama Kuu za mwaka 2009.

Kwa maoni yao, Zitto alipaswa kusajili kesi yake katika Masjala ya Mahakama ya Wilaya na sio Masjala ya Mahakama Kuu, kama alivyofanya.

Kwa mujibu wa Kibatala, katika hukumu iliyotolewa leo na Mahakama Kuu, Jaji Mziray amekubaliana na hoja hizo mbili.

Uanachama wake

Katika mkutano wake na waandishi, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, amesema kwa sasa Chadema haina mahusiano yoyote ya kisiasa na Zitto.

“Kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chadema zilizopo sasa hivi, mwanachama anayewashitaki viongozi wa chama mahakamani badala ya kufuata ngazi za kimadaraka ndani ya chama anakuwa amefanya usaliti na hivyo kupoteza sifa ya kuendelea kuwa mwanachama. Kwa hiyo, Chadema ilishamwondolea udhamini Zitto,”amesema Lissu.

Hata hivyo, mwanasheria wa Zitto, ameandika kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram kuwa taarifa kuhusu maamuzi ya Mahakama Kuu leo wamezipata kupitia mitandao ya kijamii.

“Taarifa kuhusu maamuzi ya Mahakama Kuu leo tumezipata kupitia mitandao ya kijamii kwa sababu kesi awali ilikuwa imepangwa tarehe 12.03.2015 lakini inaonekana kwenye rekodi imerudishwa nyuma na maamuzi hayo kusomwa leo bila sisi kuwa na taarifa.

“Tunafanya utaratibu tupate nakala ya maamuzi hayo ili kujua nini cha kufanya. Hatuna taarifa rasmi ya kufukuzwa Mh. Zitto Kabwe uanachama. Taratibu zote zitafuatwa pindi tukipokea taarifa rasmi kutoka mahakamani na kwenye chama. Ni matumaini yetu jambo hili halitaendeleza chuki zisizokuwa na sababu au kujenga kati ya wahusika,” amesema Msando.

error: Content is protected !!