October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yalia na NEC

Gerva Lyenda, Msemaji wa Chadema Kanda ya Pwani

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuongeza muda wa zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura, ili kufidia changamoto zilizokwamisha zoezi hilo tarehe 14 hadi 15, Februari 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea). 

Ombi hilo limetolewa leo tarehe 18 Februari 2020 na Gerva Lyenda, Msemaji wa Chadema Kanda ya Pwani, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

“Tarehe 14 siku ya Ijumaa na 15 Jumamosi kulitokea changamoto kubwa, kuachilia mbali mwitikio wa watu. Vifaa vya uandikishaji ilikuwa shida na hili lilithibitishwa na NEC kwamba mashine  zilitumiwa sehemu nyingi.

Hivyo siku mbili Ijumaa na Jumamosi zoezi lilisua kutokana na vifaa kutofanya kazi vizuri lakini lilirejea siku ya Jumapili,” amesema Lyenda.

Licha ya changamoto ya vifaa, Lyenda amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikwama kuandikishwa baada ya wasimamizi kuwakataa kutokana na sababu ambazo hazina msingi.

“Ya tatu kuna baadhi ya sehemu wafanyabishara na wafanyakazi wanakataliwa kuandikishwa, wasimamizi wasaidizi wakisaidiwa na mawakala wa vyama hasa wa CCM, walikataa kuwaandikisha kwa madai kuwa sio wakazi wa maeneo hayo. Tume ituambie hili ni daftari la wapiga kura au wakazi?” amehoji Lyenda na kuongeza:

“Sababu kama la wapiga kura fikiria wafanyabaidhara wa Kariakoo hawaishi kati kati ya mji . Anatoka nyumbani saa 11 alfajiri, anafanya kazi hadi saa 1 usiku,  nyumbani anarudi saa 3 usiku. Shughuli za maendeleo uchumi wake wa kuendesha maisha iko Kariakoo mtu huyo kwa nini anyinwe haki ya kujiandikisha Kariakoo?”

Wakati huo huo, Lyenda amedai kwamba mawakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wanaingilia zoezi hilo kwa kurekodi namba za vitambulisho vya wapiga kura.

“Mawakala wa CCM kupitia mabalozi wanauliza unaishi wapi hatukutambui hatukuandikishi. Balozi ni kiongozi wa watu wa CCM,  kwa nini ajivike mamlaka kwa mtu ambaye si CCM au hana chama cha siasa?

Wamekuwa wanarekodi namba za vitambulisho vya watu wanaojiandikisha. Wakala ana mfuata anamuomba kadi aandike namba. Watu wanafikiri anatoka NEC, sasa hatuelewi hatma ya namba kuchukuliwa au CCM wanataka nini wafanye?”

Zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, lilianza tarehe 14 na linatarajia kumalizika tarehe 20 Februari 2020.

error: Content is protected !!