May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yalia na DPP kesi ya Mbowe

Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema

Spread the love

 

CHAMA Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania-Chadema, kimemuomba Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, aache kupiga dana dana katika kesi ya kula njama za kufanya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mbowe na wenzake, Halfan Bwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya, wanakabiliwa na Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 63/2021, yenye mashtaka sita ya ugaidi, kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi, tarehe 14 Agosti 2021 na Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara, Benson Kigaila, akizungumza na wanahabari, siku moja baada ya kesi hiyo, kuahirishwa kutokana na washtakiwa hao kutofikishwa mahakamani, kwa sababu ya changamoto ya usafiri.

Kigaila ameilalamikia ofisi ya DPP, kwa kukawia kukamilisha mchakato wa kesi hiyo kuhamishiwa kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, kitendo alichodai kinasababisha mwenendo wake kuchelewa na kuwanyima haki ya washtakiwa.

“Mpaka jana inaonekana DPP hajapeleka faili mahakamani, kwa nini DPP hapeleki file Mahakama Kuu? ili wakamalizie taratibu katika Mahakama ya Kisutu ili kesi isikilizwe? Wanajua hawana kesi ya kuthibitisha mahakamani,” amedai Kigaila.

Kigaila ameongeza “ndiyo maana hawataki kufanya kesi iende mahakamani, ndiyo maana wanasema mtandao unagoma mara gari hakuna. Wanapiga danadana hapa ili mwenyekiti aendelee kuwa ndani.”
Kigaila amedai kuwa, kesi hiyo imekwama kusikilizwa zaidi ya mara mbili, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo changamoto ya mtandao, usafiri wa kuwaleta washtwakiwa mahakamani na DPP kutokamalisha mchakato wa kuifungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu, yenye mamlaka ya kusikiliza mashtaka ya ugaidi.

MwanaHALISI Online imemtafuta kwa njia ya simu, DPP Mwakitalu, kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa malalamiko hayo, ambaye ameshindwa kutoa ufafanuzi huo akisema yuko safarini.

DPP Mwakitalu ameuahidi mtandao huu kuwa, anafuatilia suala hilo kisha atatoa taarifa rasmi.

“Sina hakika kuhusu suala hilo, niko safarini ngoja nifuatilie nitakupigia,” amesema DPP Mwakitalu.

Tarehe 5 Agosti 2021, mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, iliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 6 Agosti mwaka huu, kutokana na tatizo la mtandao lililokwamisha usikilizwaji wake kwa njia ya video ‘Video onference’.

Tarehe 6 Agosti 2021, kesi hiyo iliahirishwa tena hadi Ijumaa tarehe 13 Agosti mwaka huu, baada ya upande wa mashtaka kudai kutokamilisha baadhi ya taratibu. Hata hivyo, siku hiyo kabla kesi kuahirishwa, Mbowe na wenzake walisomewa upya mashtaka na Wakili wa Serikali, Pius Hilla.

Jana Ijumaa, kesi hiyo iliahirishwa tena hadi tarehe 27 Agosti 2021, baada ya washtwakiwa kutofikishwa mahakamani kutokana na changamoto ya usafiri.

error: Content is protected !!