Monday , 29 May 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema ‘yajitutumua’ kwa Prof. Assad
Habari za SiasaTangulizi

Chadema ‘yajitutumua’ kwa Prof. Assad

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimejibu madai ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, juu ya ununuzi wa gari la chama hicho na matumizi mabaya ya fedha za umma. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, leo tarehe 13 Aprili 2019, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila, amesema kuwa Chadema hakikununua gari hilo moja kwa moja kama ambavyo CAG alivyoonesha.

Amesema, “sisi tulimkopesha fedha mwanachama wetu ambaye (jina tunalo), kwa ajili ya kununua gari hilo. Tulikubaliana kwamba atalipa fedha hizo kidogo kidogo katika kipindi cha miaka mitatu.”

CAG ameeleza katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, kuwa chama hicho kimefanya malipo ya mamilioni ya shilingi bila kuwa na nyaraka za kuthibitisha malipo hayo.

Miongoni mwa malipo yaliyofanyika; na ambayo CAG anadai hayakufuata taratibu, ni ununuzi wa gari la chama hicho, aina ya Nissan Patrol. Gari hilo lina thamani ya Sh. 147 milioni.

Anasema, “pamoja na gari hilo, kunadaiwa kununuliwa na Chadema, lakini linaonyesha kumilikiwa na mwanachama mmoja wa chama hicho; badala ya kumilikiwa na  bodi ya udhamini kama taratibu zinavyotakiwa.”

Akizungumzia sintofahamu hiyo, Kigaila amesema, Kigaila amesema, baada ya mwanachama huyo kushindwa kurejesha fedha hizo, chama kiliamua kuchukua gari lake.”

Anasema, “hivyo basi, wakati wa ukaguzi, chama kililazimika kumuonesha CAG gari hilo kama mbadala wa fedha zilizotumika.”

“Kilichotokea si kigeni kwenye vyama vyote. Kuna mwanachama aliyeomba chama kimkopeshe hela ili anunue gari. Aliahidi atarudisha fedha hiyo. CAG aliona mkataba wake,  kwamba atarudisha fedha hizo ndani ya miaka mitatu,” ameeleza.

Amesema, “…na ndio maana chama kilikuwa hakinunui gari.  Hakikuwa na shida ya gari. Aliyekuwa na shida ya gari, ni mwanachama. Tukamkopesha, lakini baada ya kuona hela ya umma inaweza kupotea, chama kikaenda kulipa kwa yule muuzaji na kikachukua gari kukaa nalo mpaka arudishe ule mkopo.

“Baada ya miaka miwili, alipoonekana hajarudisha, chama kikamuandikia barua kukatisha mkataba. Mwanachama  akabadilika. Akasema, hawezi kulipa hela, sababu biashara zake zimebadilika; chama kikachukua hilo gari.”

Hata hivyo, kinyume na maelezo ya Kigaila, kinachoelezwa na CAG katika kifungu cha 12.3.2 CAG cha ripoti yake, ni kwamba “tarehe 30 Machi 2017, Bodi ya wadhamini ya Chadema, iliingia mkataba ya AMC Tanzania Limited kwa ajili ya ununuzi wa gari jipya aina ya Nissan Patrol Y61 – GRX kwa bei ya dola za Kimarekani 63,720 (Sh. 147,760,080).”

Anasema, kifungu cha 1 cha Mkataba huo, kinaelekeza kuwa gari hilo litakalonunuliwa, lisajiliwe kwa jina la Bodi ya Wadhamini ya chama hicho.

Anasema, “kinyume na masharti yaliyomo kwenye mkataba, Ibara ya 1, gari hilo lilisajiliwa kwa jina la mbunge.

“Hata baada ya kupitia rejesta ya mali za chama, nilibaini kuwa hakuna kumbukumbu za gari aina ya Nissan Patrol, Y61 -GRX, lililosajiliwa kwenye rejesta za mali ya Chadema, pamoja na gari hilo kununuliwa na fedha za chama na kutumika na Chadema.”

Anasema, “zaidi ya hayo, gari lililonunuliwa liliingizwa kwenye taarifa za fedha za chama kama mkopo, uliotolewa kwa mbunge bila makubaliano yoyote kati ya mbunge na Bodi ya Wadhamini ya Chadema.

“Nilibaini kuwapo kwa mawasiliano ya barua kati ya mbunge na Chadema kuhusu kusitishwa kwa mkataba wa mkopo na urejeshwaji wa gari hilo. Jambo hili lilitokea, mapema tu, baada ya kutoa hoja ya ukaguzi.”

Anaongeza,“hata hivyo, wakati wa ukaguzi wangu, Februari 2019, mkataba wa mkopo huo, haukuwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi. Kwa maoni yangu, ni kwamba kuonyesha thamani ya gari kama mkopo kwa mbunge, kunapotosha watumiaji wa taarifa za fedha za chama.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Uamuzi juu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi 13 Juni

Spread the love  MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR), imepanga...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jeshi la Polisi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti

Spread the love  JESHI la Polisi Nchini limesema kuwa katika kukabiliana na...

KimataifaTangulizi

Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Spread the love  MMOJA wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya Kimbari ya...

Habari za Siasa

Musoma Vijijini waomba ujenzi wa barabara uanze haraka

Spread the loveJIMBO la Musoma Vijijini, mkoani Mara, limeomba Serikali kuhakikisha ujenzi...

error: Content is protected !!