January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yaishushia tuhuma CCM

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelaani vitendo vya vurugu vinavyochochewa na viongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Kauli hiyo imetokana na kitendo kilichotokea jana katika Halmashauri ya Kilombero kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali aliondolewa kwenye ukumbu wa mkutano kwa kukokotwa na polisi baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, Azimina Mbilinyi kutoa amri atolewe nje.

Sababu za kutolewa mbunge huyo zilielezwa kuwa hakupaswa kuwepo na kushiriki upigaji kura ambapo mwenyekiti huyo alidai amepokea maelekezo hayo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye Makao Makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu chama hicho, Salim Mwalimu amesema, kitendo alichofanyiwa Lijualikalini ni cha uzalilishaji.

“Naamini kwamba matukio yanayofanywa katika halmashauri ambazo Ukawa tumeshinda yanapangwa na CCM kwa kushirikiana na serikali yake.

“Kwanini matukio ya uzalilishaji yafanyike kwenye maeneo ambayo sisi tumeshinda na si maeneo ambayo wao wameshinda?” amehoji Mwalim.

Mwalim amesema, Halmashauri ya Kilombero inaongozwa na Ukawa kutoka na kuwa na madiwani na wabunge wengi kuliko CCM na kwamba uchaguzi huo umeghairishwa kwa mara ya tatu. CCM wana madiwani pamoja na wabunge viti maalumu 18 huku Ukawa wakiwa na 20.

“Pamoja na ushindi wa Ukawa kuonekana waziwazi lakini bado CCM wanaleta filigisufiligisu ya kuleta hata wabunge wa nje ilimradi tu washinde.

“Hawataweza kutushinda hata kwanini maana hata sisi tukipeleka wabunge toka nje bado tutawapita. Na hiyo ni ishara ya kutuogopa,” amesema Mwalimu.

Hata hivyo, Mwalim amesema kutokana na kitendo alichofanyiwa mbunge huyo jana wanaitaka serikali kulichukulia uzito suala hilo na kuhakikisha mkurugenzi huyo aliyetoa amri kwa polisi kutumia mabavu kumtoa nje mbunge huyo achukuliwe hatua za kinidhamu.

Pia, wamemtaka mkurugenzi huyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kuonesha barua aliyotumiwa na Simbachawene ya kutoa amri ya kumtoa nje mbunge huyo.

Mbali na hilo, pia ametoa rai kwa serikali kufuata misingi bora ya uongozi haswa katika kusimamia masuala ya nayowahusu wananchi hususani suala la Meya wa Jiji ambalo bado halijafanyika.

error: Content is protected !!