VYAMA vya siasa nchini Tanzania, vimefanya uteuzi wa wagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 huku idadi ya wanawake ikiwa hairidhishi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF) na ACT-Wazalendo vimekwisha kamilisha uteuzi wa wagombea wao wa ubunge wa majimbo.
Jumla ya majimbo 264 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yatahusika kwenye uchaguzi mkuu kwa maana ya majimbo 214 ya Tanzania Bara na 50 Zanzibar.

Katika uteuzi uliofanywa na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapindizi (CCM), kwenye majimbo 264, imeteua wanawake wasiozidi 25 kugombea kwenye majimbo.
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, katika majimbo 264 ya uchaguzi, ina wagombea wanawake zaidi ya 50.
Soma zaidi hapa
Sera kabambe ya wanawake, wenye ulemavu na vijana yaandaliwa
Chama cha Wananchi (CUF), katika uteuzi uliotolewa leo Jumatatu kwenye majimbo 136 ya Tanzania Bara, imeteua wanawake zaidi ya 30 kusimama majimboni.
ACT-Wazalendo ina wagombea zaidi ya 20.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee akizungumza katika Mkutano Mkuu wa chama hicho mwezi uliopita, alisema wamejipanga kuhakikisha wanatoa ushindani mkubwa majimboni.
Mdee ambaye anagombea ubunge Kawe jijini Dar es Salaam alisema, wanawake ni jeshi kubwa, wakiaminiwa wanaweza kufanya mapinduzi na wamekuwa na msimamo wa kutotohama hama.

Mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda alisema ushiriki wa wanawake, vijana na wenye ulemavu umekuwa hauridhishi.
Alisema, kutokana na hilo, Jukata kwa kushirikiana na Ushiriki Tanzania wanaandaa sera ya kitaifa ya ushiriki wa makundi hayo kwenye siasa ili kuwapo na uwiano sawa.
Mwakagenda alisema, wanawake hawapewi kipaumbele kwenye majimbo badala yake wanaelezwa wasubiri kugombea viti maalum jambo ambalo linaleta shida, hivyo vyama vya siasa vinapaswa kutoa haki sawa kwa wanaume na wanawake.
Alisema, sera hiyo iliyokusanya maoni ya wadau mbalimbali, itakapokamilika itawasilishwa serikalini kwa utekelezaji ili kuwezesha kufikia ile 50 kwa 50.
Leave a comment