CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Serikali itoe ripoti ya mapato na matumizi ya fedha zilizotokana na madini yaliyochimbwa katika kipindi cha miaka 20 mfululizo, ili wananchi wajue wamenufaikaje na rasilimali hiyo. Anaripoti mwandishi Wetu, Mara … (endelea).
Wito huo umetolewa leo tarehe 23 Januari 2023 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tarime Mjini, mkoani Mara.
“Tarime uchumi wake unategemea madini, kunapaswa kuwe na mikakati ya dharura, moja Serikali itoe ripoti ya miaka 20 ya uchimbaji katika Mgodi wa North Mara, mapato kiasi gani yametumika, wananchi wamenufaika namna gani,”
“Pili, Serikali ieleze ukweli wananchi ni lini mapato yatasimama kwa sababu ya kuisha kwa dhahabu, tatu Serikali iwaambie Tarime mazingira gani inaweka kwa kushirikiana na sekta binafsi kuwa na uchumi mbadala baada ya madini kuisha,” amesema Mnyika.
Katika hatua nyingine, Mnyika amewataka wananchi wa Mara kupigania ajenda ya upatikanaji wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, ili kupata Serikali inayotatua changamoto zao.
“Taifa letu linahitaji katiba na tume huru ya uchaguzi, Mwenyekiti Mbowe ametuongoza kwenye mazungumzo ya maridhiano hatimaye uhuru wa kisiasa wa kufanya mikutano ya hadhara umefunguliwa, uhuru huu ni hatua moja ya ushindi lakini hatua kubwa tunayopaswa kupigania na kukamilisha ni mchakato wa katiba ili kabla ya 2025 Tanzania iwe na katiba mpya,” amesema Mnyika.
Katibu Mkuu huyo wa Chadema amesema kuwa, katiba mpya itakapopatikana itasaidia wananchi kupata viongozi wenye sifa ambao watasaidia kulinda maslahi yao na ya nchi kwa ujumla.
KUMEKUCHA
Katiba mpya ni muhimu sana wakati huu! Je kama watanzania tumejiuliza vitu,mambo muhimu yanayoitajika kuwemo ndani ya katiba yetu mpya?-katiba ni dira,muongozo usichezewe-kisiasa,binafsi,kidini! Tulijue hilo oou…!