Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema yaihoji NEC ‘karatasi za kura, mfumo wa kujumlisha matokeo
Habari za SiasaTangulizi

Chadema yaihoji NEC ‘karatasi za kura, mfumo wa kujumlisha matokeo

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, imetakiwa kuweka wazi mambo mbalimbali yahusuyo Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020 ikiwemo kampuni itakayotumika kuchapisha karatasi za kura na mfumo wa ujumlishaji matokeo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)

Pia, NEC imetakiwa kutoa daftari la kudumu la wapiga kura linaloonyesha jina na picha za wapiga kura na nakala ya karatasi ya matokeo ya kura itakavyokuwa ambayo kila wakala wa mgombea anatakiwa kupewa.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi tarehe 10 Oktoba 2020 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali ya uchaguzi.

Mnyika amesema, Jumatano ya tarehe 8 Oktoba 2020, NEC iliitisha kikao cha kwanza cha Kamati ya Kitaifa cha Manunuzi na Logistiki “yaani toka mchakato wa uchaguzi ulipoanza, NEC imekuwa ikifanya manunuzi na logistiki peke yake na 8 Oktoba ndiyo ikafanya kikao cha kwanza.”

Amesema, kulikuwa na taarifa kwamba kampuni itakayochapisha karatasi za kupigia kura ni kutoka Afrika Kusini na kwa sasa wanataarifa kampuni moja ya jijini Dar es Salaam imepewa jukumu la kuchapisha karatasi hizo.

“NEC ijitokeze hadharani ieleze ni kampuni gani kati ya ile ya Afrika Kusini au ya Dar es Salaam Tanzania itakayochapisha karatasi za kura, ieleze kwa umma ni mchakato gani ulifanyika kuipata kwani hiyo ya Dar es Salaam kati ya wamiliki wake wako makada wa CCM,” amesema Mnyika

“Usipokua na usalama wa kura, unaweza kuchapisha karatasi nyingi za ziada, kwa hiyo NEC ijitokeze sasa ivihakikishie vyama na Watanzania, kampuni gani inahusika na uchapishaji kura,” amesema

Mnyika amekumbushia kile kilichowahi kujitokeza nchini Kenya kwa Mahakama kuzuia moja ya kampuni iliyokuwa imepewa zabuni ya kuchapisha karatasi kutokana na kuwa na uhusiano na mmoja wa wagombea urais.

“Jambo hili lisichukuliwe kwa wepesi, Kenya mwaka 2007 waliingia kwenye mgogoro wa suala hili na Mahakama ya Kenya iliikatalia tume ya uchaguzi kwa sababu mahakama imeona mzabuni aliyeteuliwa ana mahusiano na mgombea wa urais kwenye mchakato wa urais.”

“Suala la karatasi za kupigia kura ni nyeti. Katika kikao hicho cha 8 Oktoba cha manunuzi na logistiki, vyama havikuelezwa chochote,” amesema

Pia, Mnyika ameitaka NEC kutoa daftari la kudumu la wapiga kura kwa vyama vyote ili waweze kulichambua na kuona uhalali wake “lakini mpaka sasa hawajatoa, zaidi ya kutupa ‘flash’ yenye orodha ya majina. Kuna tofauti kati ya orodha na daftari lenyewe.”

“Mpaka tunazungumza, haijatoa nakala ya daftari la kudumu la mwisho la wapiga kura. Orodha ya wapiga kura siyo daftari la kudumu la wapiga kura, tunataka hilo daftari ili kuona jina na picha ya mpiga kura na sisi tutalitazama na kuona hakuna wapiga kura hewa na hili ndilo tutalitumia kuwapa mawakala wetu ili kulinganisha siku ya upigaji kura,” amesema

Mnyika amesema, tume hiyo inapaswa kuweka wazi mfumo wa kujumlisha kura kwa vyama vya siasa ili viweze kuukagua na utakavyofanya kazi.

“Katika kikao cha kamati ya kitaifa cha manunuzi na logistiki, haijaweka wazi masuala ya mfumo wa ujumlishaji wa matokeo kutoka katika majimbo na taifa. NEC inatarajia kuanza mafunzo juu ya mfumo huu, tunataka kabla ya mfumo huu haujaanza kutoa mafunzo, vyama tupewe fursa kuona na kuutazama utakavyofanya kazi,” amesema Mnyika

Katibu mkuu huyo amesema, wamepeleka malalamiko kwa Tume juu ya ukiukwaji wa kanuni za maadili uliofanywa na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Pombe Magufuli alioufanya tarehe 8 Oktoba 2020.

Mnyika amesema, siku hiyo, Rais Magufuli alitumia shughuli ya kiserikali ya uzinduzi wa kituo cha kimataifa cha mabasi Mbezi Mwisho Dar es Salaam kujipigia kampeni yeye mwenyewe na wagombea wa chama chake kinyume na kanunizi hizo.

“Tumepeleka malalamiko NEC kulalamikia hili. Katika uzinduzi wa kituo cha mabasi mbezi, nje ya ratiba ya kampeni alifanya kampeni ya kwake binafsi na ya wagombea wengine.”

“Alitumia rasilimali za umma kufanya kazi ya CCM, logistiki hazikuwa za CCM zilikuwa za Serikali na tumepeleka malalamiko haya. Tukio lilitokea 8 Oktoba na jana 9 Oktoba tumepeleka, hili ni jaribio kwa NEC kuona kama itatenmda haki,” amesema Mnyika

Pia, wamepeleka malalamiko kwa kamati hiyo kulalamikia utendaji wa jeshi la polisi na kumwandikia barua rasmi Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro juu ya askari wake kutowatendea haki ikiwemo kukamata timu za kampeni za wagombea wake wa ubunge kinyume na taratibu za uchaguzi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali yawaangukia viongozi wa dini

Spread the loveSERIKALI imewaomba viongozi wa dini, waendelee kuelimisha wananchi kudumisha amani...

Habari MchanganyikoTangulizi

Afya ya akili yatajwa chanzo kuvunjika ndoa

Spread the loveCHANGAMOTO ya afya ya akili, imetajwa kuwa chanzo cha migogoro...

Habari za Siasa

Azzim Dewji aitaka Serikali iwanyooshe mafisadi

Spread the loveMFANYABIASHARA maarufu nchini, Azzim Dewji, ameitaka Serikali iwachukulie hatua wezi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

error: Content is protected !!