December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yaibua kasoro 10 uamuzi kesi ya Mbowe, wenzake

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibua hoja zaidi ya kumi, kuhusu kasoro zilizojitokeza kwenye uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, mkoani Dar es Salaam, dhidi ya kesi ndogo katika kesi ya msingi, inayomkabili Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hoja hizo zimeibuliwa leo Alhamisi, tarehe 21 Oktoba 2021 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akizungumza na wanahabari, mkoani Dar es Salaam. Siku moja baada ya mahakama hiyo kutoa uamuzi katika kesi hiyo ndogo, uliotupilia mbali mapingamizi ya Mbowe na wenzake.

Waliyoweka dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adam Kasekwa, wakitaka yasitumike kama ushahidi wa jamhuri mahakamani hapo, wakidai yalichukuliwa kinyume cha sheria.

“Kwa kweli ni uamuzi ambao umeiabisha mahakama kwa namna ambavyo maamuzi haya yametolewa, inabidi mahakama ichukue hatua ya kujinasua. Isilifanye hili suala likawa la Jaji siyani peke yake. Atapangiwa jaji mwingine atafanya haya, halafu mhimili wa kutoa haki unazidi kuporomoka,” amesema Mnyika.

Katika kesi hiyo ndogo, mawakili wa Mbowe na wenzake, walipinga maelezo hayo ya onyo wakidai mtuhumiwa huyo alihojiwa nje ya muda kisheria, pamoja na kuchukuliwa maelezo ya onyo baada ya kuteswa.

Lakini, mahakama hiyo jana tarehe 20 Oktoba 2021, mbele ya Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani, iliyatupa mapingamizi hayo ikisema kifungu namba 50 (2) na cha 51, cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2019, vinaruhusu muda wa kumhoji mtuhumiwa kuongezwa kwa sababu maalum, ikiwemo za upelelezi.

Wakati ukitoa ushahidi wake, upande wa jamhuri ulidai ulichelewa kumhoji mtuhumiwa mkoani Kilimanjaro, kwa kuwa alikuwa anawasaidia kumtafuta mtuhumiwa mwenzao, Moses Lijenge, pamoja na kesi yao kufunguliwa mkoani Dar es Salaam.

Pia, uamuzi huo wa Jaji Siyani, ulisema hakuna mahali mtuhumiwa huyo wakati akitoa ushahidi wake, alipinga kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Bali alisema alitoa maelezo baada ya kuteswa , katika Kituo cha Polisi Mbweni mkoani humo, hivyo mapingamizi hayo hayana mashiko.

Jaji Siyani alisema, upande wa utetezi ulipaswa kupinga kitabu cha mahabusu ‘Dentetion Register’, kilicholetwa na jamhuri kama sehemu ya ushahidi wake, ambacho kinaonesha taarifa za mtuhumiwa huyo kufikishwa ha kuhojiwa kituoni hapo.

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema

Kufuatia hoja hizo, Mnyika aliibua hoja zaidi ya kumi, akidai kwamba zinaonesha kuwa Jaji Siyani alitoa uamuzi huo huku akiacha ushahidi wenye mashaka.

Hoja ya kwanza iliyoibuliwa na Mnyika, ni madai ya kwamba Jaji Siyani alishindwa kupima ushahidi ili kujiridhisha kama hauachi mashaka, kulingana na misingi ya mashauri ya jinai, akidai alipaswa kujiridhisha kama maelezo hayo ya onyo ni halali ama sio halali.

“Jaji hakuongozwa na msingi wa kwamba kwenye mashauri ya kijinai, ushahidi unapimwa kwa ushahidi bila mashaka yoyote, huu msingi haukumuongoza hususan katika jambo kama hili linalokubaliwa au kataliwa kuhusu maelezo ya onyo,” amesema Mnyika.

Mnyika amedai “matokeo yake jaji ameegemea katika maelezo ya upande mmoja, bila kuchunguza usahihi wake au kutokuwa na usahihi wake. Akaacha kusikiliza uzito wa maelezo na ushahidi wa upande wa utetezi .”

Hoja zingine mbili zilizoibuliwa na Mnyika kuhusu uamuzi huo, zilidai kwamba Jaji Siyani hakuzingatia hoja ya mtuhumiwa kuhojiwa nje ya muda, pamoja na kuchukuliwa maelezo ya onyo baada ya kuteswa haikuzingatiwa .

Hoja ya nne iliyoibuliwa na Mnyika, ilidai Jaji Siyani hakufanyia kazi malalamiko ya utetezi dhidi ya Jeshi la Polisi, kutochukua maelezo ya mtuhumiwa huyo mkoani Kilimanjaro, kama lilivyofanya kwa watu walioshuhudiwa wakati anakamatwa mkoani humo.

“Wakati jamhuri unasema waliacha kuandikisha maelezo sababu walikuwa wanazunguka na mtuhumiwa kumtafuta mtuhumiwa mwingine, kwa nini wadada wawili walioandikishwa ushahidi Moshi hawakusafirishwa kuja Dar es Salaam, wameandikishiwa Moshi?” amesema Mnyika.

Mnyika amesema hoja ya tano ni, Jaji Kiongozi Siyani katika uamuzi wake, hakuzingatia maelezo ya mshtakiwa yaliyokanusha kuhusika katika utafutaji wa Lijenge, akidai kwamba alipaswa kuchambua ushahidi huo na kuutolea uamuzi.

Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani

Hoja ya sita iliyoibuliwa na Mnyika, ilidai Jaji Kiongozi Siyani hakufanyia kazi madai ya mtuhumiwa kwamba alishikiliwa kinyume cha sheria pamoja na kuteswa, tangu alipokamatwa tarehe 5 Agosti 2020, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Hadi alivyofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, tarehe 19 Agosti mwaka jana.

Hoja ya saba iliyoibuliwa na Mnyika, imedai Jaji Kiongozi Siyani katika uamuzi wake, hakutaka kuhoji sababu za mtuhumiwa kutolewa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Mbweni, mkoani Dar es Salaam.

“Hoja hii ingechambuliwa mambo yangedhihirika kuhusu maelezo kuchukuliwa nje ya muda kisheria, ushahidi wa kimazingira ungeweza kuthibitisha kwamba watuhumwia waliteswa,” amesema Mnyika.

Hoja ya nane iliyoibuliwa na Katibu Mkuu huyo wa Chadema, ilidai Jaji Kiongozi Siyani kutumia kitabu cha mahabusu kilicholetwa na upande wa mashtaka kama sehemu ya ushahidi wake, bila kujiridhisha kama ni halali.

“Jaji amejaribu kutumia kinachoitwa kitabu cha mahabusu kuhalalisha kwamba mtuhumiwa alitoa maelezo yake kituoni hapo, hii ilitumika kuhalalisha na kujenga hoja kwamba hiki kielelezo hakikuhojiwa wakati wa mwenendo wa kesi, lakini mke wake Lilian Kibona alikwenda kituoni hapo na kuangalia kitabu cha mahabusu jina la mume wake halikuwapo,’” amesema Mnyika.

Hoja ya tisa iliyoibuliwa na Mnyika, imedai katika uamuzi wake Jaji Kiongozi Siyani hakuzingatia madai ya mtuhumiwa kuteswa, kabla na wakati wa kuandika maelezo ya onyo.

Mwanasiasa huyo ameibua hoja ya kumi, iliyodai kwamba Jaji Kiongozi Siyani hakuzingatia ushahidi wa kimazingira au ushahidi halisi, ulioonesha kwamba mtuhumiwa aliteswa.

Hoja ya mwisho iliyotolewa na Mnyika, ilidai kwamba upande wa jamhuri haukuleta mahakamani hapo ushahidi unaonesha sababu za kuchelewa kumhoji mtuhumiwa.

error: Content is protected !!