Kwamba, Jeshi la Polisi halijajibu ombi lake ama kumuhakikishia usalama wake pale ataporejea nchini. Kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa Lissu yupo nje ya nchi baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana jijini Dodoma tarehe 7 Septemba 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi tarehe 25 Juni 2020, jijini Dar es Salaam John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema amesema, Lissu bado hajahakikishiwa usalama wake na Jeshi la Polisi.
Mnyika amedai, mara kadhaa viongozi wa Chadema wamemuandikia barua IGP Simon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, kwa ajili ya kuomba ulinzi wa Lissu wakati ataporudi lakini hawajajibiwa.
Amesema, ukimya wa polisi kuhusu usalama wa Lissu, umesababisha mwanasiasa huyo aliyeko ughaibu kutorejea nchini, licha ya kukamilisha matibabu yake.

“IGP yeye binafsi hajajibu iwe kwa barua au hadharani tangu tarehe 23 Disemba 2019, nilimuandikia barua rasmi kuomba ulinzi wa polisi kwa ajili ya makamo mwenyekiti ambaye amekuwa akiishi nje ya nchi kwa matibabu tangu Septemba 7 2017,” amesema Mnyika na kuongeza:
“Lissu amekamilisha matibabu yake, na sasa licha ya kuandika barua na kukumbusha Januari 7 mwaka huu bado hujapatia majibu ya ombi letu, kimya chako hakipendezi IGP.”
Lissu kwa sasa yuko nchini Ubelgiji, alikokwenda kufanyiwa matibabu, baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma.
Hata hivyo, Mnyika amesema Chadema inaendelea kushirikiana na Lissu kuangalia namba gani watakavyoshughulikia safari yake ya kurejea nchini.
“Kutojibiwa na IGP haiwezi kuwa kikwazo, sisi kama chama kwa kushirikiana na Lissu tutalishughulikia hili jambo, kwa kuwa IGP amejitokeza mbele ya habari kuzungumzia ujio wa Lissu, aulizwe aeleze kwa nini hajajibu barua ya Mbowe kuhusu Lissu kuhakikishiwa usalama wake,” amesema Mnyika.
Leave a comment