KUSHAMIRI kwa vituko, ghiliba na mikasa ya kuogofya, kwenye zoezi la uchukuaji fomu za kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kumeisukuma Chadema kubisha hodi Ikulu. Anaripoti Kamtote Martin … (endelea).
Chama hicho, kimemwoma Rais Joh Magufuli kuingilia kati mchakato wa uchukuaji fomu, baada ya wagombea wake wengi kutupwa nje kwa kile walichoita hujuma. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019.
“TAMISEMI iko chini ya ofisi ya rais. Tunamtaka aingilie kati jambo hili, na mara zote amekuwa akisema chama chake kimefanya mambo mazuri. Aruhusu watu waingie kwenye uchaguzi.
“Kama wamefanya vizuri, wanaogopa nini uchaguzi wa serikali za mitaa? Uchaguzi huu ungekuwa kama kioo, kikikuonesha kwamba ni mchafu usoni hupaswi kugombana na kioo tumia kioo kusafisha,” amesema John Mrema, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Uenezi wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 5 Novemba 2019, katika Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mrema amesema, wagombe wa Chadema wameenguliwa katika hatua ya awali kwa mikakati maalum ya kuwadhoofisha.
Aidha, Mrema amesema matokeo ya uchaguzi huo yatampa ujumbe wa wananchi, utakaomuwezesha kubadili sera zake.
“Aingilie kati, huu uchaguzi utamsaidia yeye na serikali yake, unaweza kumsaidia kubadili sera, sababu atapata ujumbe kutoka kwa wananchi wake wa mtaa na kata,” amesema Mrema.
Hata hivyo amesema, chama hicho kitachukua hatua za dharura kukabiliana na changamoto ya wagombea wake katika uchaguzi wa serikali za mitaa kutoka na kuenguliwa.
Amesema, chama hicho kitaitisha mkutano wa dharura ambao utatangaza hatua nzito.
“Kwa kaunzia kesho, tumekubaliana sekretarieti ya kamati kuu itakaa tutakutana, lakini pia leo jioni viongozi wakuu wanakutana kwa dharura.
Pia, ametoa wito kwa wagombea wake walioenguliwa, kufuata utaratibu wa kupinga hatua hiyo, kwa kukata rufaa kwa mamlaka husika.
“Kwa sababu sisi tunapenda kufuata utaratibu, tumeaaelekeza wagombea wote kuweka mapingamizi ya kuenguliwa kwao. Hii ni utaratibu kama tukifuata hatua za kwenda mbele mahakamani, tuwe tumefuata taratibu zote,” amesema Mrema.
Leave a comment