July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yabaini rafu za CCM uchaguzi wa Meya Ilala, Kinondoni.

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimebaini njama zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na viongozi wa serikali za kutaka kuharibu uchaguzi wa Mameya na uapishwaji wa madiwani wa Wilaya ya Kinondoni na Ilala. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Kufuatia hali hiyo Chadema kimemtaka Rais John Magufuli kuingilia suala hilo kwani taasisi zote zipo chini yake hivyo awasaidie wananchi wa Dar es Salam kupata haki yao.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam  na Kaimu Katibu Mkuu Chadema Salim Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kuwa, CCM wamepania na wameaza harakati za kuhujumu uchaguzi wa mameya.

Mwalimu amesema, CCM wamepanga kuwapeleka Mawaziri wapya walioteuliwa na kuapishwa na Rais Magufuli katika zoezi la upigaji kura wa Mameya, kitendo ambacho hakijawahi kutokea.

“Kwa kufanya hivyo watakuwa wanavunja taratibu na sheria za nchi, tumepata taarifa pia kuna vikao vimekaliwa juzi kati ya viongozi wakuu wa CCM na waserikali ili kupanga mikakata ya kuwarubuni wakurugenzi. Wakurugezi wa Halmashauri pia wanaonekana kuunga mkono kwani hata jana waliitwa kupewa mbinu za kutuhujumu.

Ameeleza, pia kuna taarifa wamepata kwamba CCM  wameshapanga tarehe ya kufanyika kwa zoezi hilo ambapo imevuja kuwa ni Januari 5 huku Chadema wakilalamikia kutopewa taarifa rasmi.

” Tunajua kwamba wamefanya hivyo kwa makusudi ili watushitukize. Pia wamepanga kujaza maaskari na silaha ndani ya uchaguzi ili kututisha. Kama watafanya hivyo sisi tutawaita wananchi kwani hatutakubali itokee kama ya Tanga.”

Aidha, ameongeza yanayofanywa sasa na CCM ni ishara ya kushindwa. Pia Mwalimu ameeleza kusikitishwa na ukimya wa Rais Magufuli kana kwamba hajui wala haoni kinachoendelea.

Mwalimu ametoa wito kwa Rais Magufuli pamoja na uongozi wa CCM kusitisha kwa haraka mbinu zote chafu wanazoendelea kupanga dhidi yao, na kuwataka kukubali matokea na kuheshimu kura za wananchi.

error: Content is protected !!