August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yaanza safari mpya

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza safari mpya ya kudai haki ya kufanya mikutano ya hadhara, anaandika Moses Mseti.

Tayari chama hicho kimefungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ya kuiomba mahakama kupiga marufuku Jeshi la Polisi nchini kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani.

Chadema chini ya Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, kimekwenda mahakamani kuwashitaki Wakuu wa Polisi wa Wilaya za Geita na Kahama, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Polisi Makao Makuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hivi karibuni, chama hicho kilitangaza kufanya mikutano ya hadhara ya kuishtaki serikali kwa wananchi kutokana na kuendesha nchi bila kufuata kanuni na sheria pamoja na kuzuia kuoneshwa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge.

Hata hivyo, baada ya Chadema kutangaza kufanya oparesheni hiyo iliopewa jina la ‘Okoa Demokrasia Nchini’ Polisi kupitia kwa Kamishna wa Mafunzo wa Polisi, ilizuia kufanyika kwa mikutano hiyo kwa kile ilichodai, hali ya usalama kuwa tete nchini.

Hatua ya polisi kuzuia mikutano hiyo kilipingwa na chama hicho kikuu cha upinzani.

Mbowe akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2016 jana amesema kuwa, wamelazimika kufungua kesi hiyo baada ya kuminywa kwa Demokrasia na wao kuzuiliwa kufanya mikutano ya kuelimisha wananchi.

Amesema kuwa, wamefungua kesi hiyo kwa lengo la kuiomba mahakama kupiga marufuku polisi kuzuia mikutano yao na badala yake wanapaswa kulinda mikutano hiyo kwani kazi yao ni kulinda raia na mali zao kama sheria inavyoelekeza.

“Kazi ya chama cha siasa ni kutoa mawazo mbadala na kuhamasisha wananchi kudai haki yao lakini sasa polisi na viongozi wao wanaotaka kuzuia nguvu ya upinzani nchini ili wao waonekane kila mahara haiwezekani hiyo ni lazima watu wadai haki yao.

“Tumeona hata bungeni wanavyofanya mbinu ya kutaka kuzima nguvu ya upinzani na sasa wameanza kuhamia na kwenye mikutano ya hadhara baada ya kuona nguvu ya upinzani ni kubwa sana nje na ndani ya bunge,” amesema Mbowe ambae pia ni Mbunge wa Hai.

Katika ufunguzi wa shauli hilo, Mbowe aliambata na viongozi wengine wakitaifa wakiwamo, Salim Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Chadema- Zanzibar, Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Pastrobas Katambi, Mwenyekiti wa Bavicha na wabunge wa chama hicho.

Akizungumzia kuteswa viongozi wa Ukawa Mbowe amesema kuwa, tangu uchaguzi mkuu wa mwaka jana kumalizika, kumejitokeza mambo mengi ikiwemo ya viongozi wa chama hicho kuteswa na polisi kwa shinikizo la Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema kuwa, Serikali ya CCM inalazimika kufanya vitendo hivyo baada ya uchaguzi wa mwaka jana vyama vya upinzani kuungwa mkono na wananchi hivyo wanataka kuzuia mikutano hiyo ili kuua nguvu ya upinzani.

Amesema kuwa, Serikali ya Rais John Magufuli imeanza kuhaha na kutaka kuzuia nguvu hiyo ya upinzani ili wao waendelee kuendesha nchi kwa mabavu bila kufuata sheria za nchi pamoja na ‘kuuza’ sura kwenye magazeti.

“Rais (John Magufuli) na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) wao wanataka waonekane kwenye magezeti na Televisheni kila siku na sasa wanataka kuzuia vyama vingine vya siasa kufanya kazi zao,” amesema Mbowe.

error: Content is protected !!