CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitapigania marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 ili vifungu vinavyodhoofisha uhuru wa tasnia hiyo viondolewe. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Kauli hiyo iliyolewa jana tarehe 15 Januari 2023 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, kuhusu ratiba ya utekelezaji wa mikutano ya hadhara ya chama hicho.
Mwanasiasa huyo alisema kuwa, maudhui yanayotolewa katika mikutano ya hadhara hayatafikia umma inavyostahili, endapo sheria zinazozibana vyombo vya habari hazitafanyiwa marekebisho.
“Kati ya sheria ambazo tunafikiri ni sheria za awali za kufanyiwa marekebisho au kuandikwa upya ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari sababu huwezi kurudi kwenye mikutano kama umevifunga vyombo vya habari mikono,” alisema Mrema na kuongeza:
“Mikutano hiyo haitawafikia wananchi, kwa hiyo tunadhani kati ya sheria ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho na ikiwezekana kwenye Bunge linalokuja la Februari ni sheria ya habari pamoja na sheria ya makosa ya mtandao.”
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetangaza kusudio lake la kuwasilisha bungeni jijini Dodoma, Muswada wa Marekebisho ya sheria hiyo, Januari mwaka huu.
Leave a comment