October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema watinga kwa msajili wafuasi wake kukamatwa, ajibu

Jaji Francis Mungi, Msajili wa Vyama vya Siasa

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani nchini Tanzania, kimemuomba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, aingilie kati suala la kushikiliwa kwa wanachama na wafuasi wake na Jeshi la Polisi Kinondoni, Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumatatu, tarehe 4 Oktoba 2021 na Afisa Habari wa Chadema Kanda ya Pwani, Gerva Lyenda, akizungumza na wanahabari mkoani Dar es Salaam.

“Katika mazingira kama hayo tulitegemea msajili atoke hadharani alikemee jeshi, kwamba jamani mnachokifanya mnavuka mstari. Mnakiuka sheria ya vyama vya siasa ambayo ndiyo anailinda. Tunatoa wito kwa msajili aingilie kati tunaonewa na Jeshi la Polisi,” amesema Lyenda.

Aidha, Lyenda amesema wafuasi hao wa Chadema wanaoshikiliwa katika Kituo cha Polisi Mbweni, mkoani Dar es Salaam, wamegoma kula tangu jana hadi leo, wakishinikiza waachwe huru bila masharti au wafikishwe mahakamani.

“Sisi tumeamua tusihangaike na polisi, wale mahabusu wote tisa kuanzia jana wamegoma kula chakula. Wameshinda njaa tangu jana hawajala na leo wameamka hawajala na wamesema hatutakula mpaka mtuachie bila masharti yoyote au mtupeleke mahakamani,” amesema Lyenda.

MwanaHALISI Online limemtafuta Jaji Mutungi ili kupata msimamo wake kuhusu suala hilo, ambaye alijibu akisema hajapata malalamiko hayo na kwamba ameyasikia kwa mara ya kwanza kutoka kwa mwandishi wa mtandao huu aliyempigia simu.

Gerva Lyenda, Msemaji wa Chadema Kanda ya Pwani

Jaji Mtungi amesema, akipata taarifa hizo rasmi kutoka Chadema, atatuma vijana wake wakazifanyie kazi.

“Wewe ndiye unayeniambia kuhusu taarifa hizo, mimi sijaambiwa na mtu yeyote  wala sina habari. Ni vyema hicho wanachokisema uambiwe, nikiambiwa nitaelekeza vijana wangu wafuatilie kujua hicho wanachokisema,” amesema Jaji Mutungi.

Wanachama hao wa Chadema na mwandishi wa habari wa televisheni ya mtandao ya Mgawe, Harlod Shemsanga, wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mbweni, mkoani Dar es Salaam tangu Jumamosi iliyopita.

Baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi Kinondoni, wakifanya mazoezi ya viungo (Jogging), kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe mkoani humo.

Walikamatwa na Jeshi la Polisi, kwa tuhuma za kufanya vitendo vyenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kutengeneza hisia zenye mitizamo ya kisiasa kupitia kivuli cha mazoezi.

error: Content is protected !!