Sunday , 3 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema wasusia Uchaguzi Serikali za Mitaa
Habari za SiasaTangulizi

Chadema wasusia Uchaguzi Serikali za Mitaa

Viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe katika kikao cha dharura kilichofanyika jijini Dodoma
Spread the love

KAMATI Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewaamuru wanachama, viongozi na wafuasi wake, kujiondoa katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, leo tarehe 7 Novemba 2019, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema, chama chake kimechukua hatua hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa uchaguzi huo, ulitawaliwa na “udanganyifu, ghiriba na upendeleo.”

Amesema, Chadema haitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, kufuatia serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwatumia watendaji wa mitaa, kuwafanyia uharamia wagombea wao.

Akiongea kwa hisia kali, Mbowe alisema, “Kamati Kuu ya Chadema, imeamuru wanachama wake wote, viongozi na wafuasi kote nchini, kususia kwa kadri wanavyoweza, zoezi linaloendelea sasa la uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.”

Mbali na kususia uchaguzi huo, Chadema kimewataka wanachama na wafuasi wake hao, kutowatambua viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo.

Uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, unatarajiwa kufanyika nchini kote, tarehe 24 Novemba mwaka huu.

Amesema, serikali kwa ushirikiano na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeunajisi uchaguzi huo kwa kiwango ambacho hakiwezi kuusafisha.

Amesema, kutokana na hali hiyo, Chadema kimeamua kutoshiriki uchaguzi huo kwa kuwa kuendelea kushiriki, ni sawa na kubariki haramu inayotaka kugeuzwa halali.

Kufuatia uamuzi huo, Mbowe amesema, chama chake, kinawataka wanachama, viongozi na wagombea wake wote walioenguliwa, kusitisha zoezi la kukata rufaa.

“…wagombea wetu wote, ni sharti wajitoe.  Kamati Kuu imesema, hatutawatambua viongozi wowote watakaopatikana kwa unajisi wa mchakato huu na hatutawapa ushirikiano,” ameeleza mwenyekiti huyo.

Amesema, Chadema kama chama kikuu cha upinzani nchini, kilitambua umuhimu wa uchaguzi huo; waliona kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza.

 “Tuliwaandaa wagombea wetu na tulitimiza taratibu zote za uchaguzi ndani ya chama. Katika hili, tulifanikiwa kwa asilimia 85 na hata baada ya kufanyiwa mizengwe, bado walifikia asilimia 60.  Lakini cha kuishangaza, hadi jana wagombea wetu wameenguliwa hadi kufikia asilimia tisa (9),” ameeleza.

Amesema, kutokana na hali hiyo, Chadema kiliamua kuitisha Kamati Kuu pamoja na wabunge ili kuweza kubadilishana mawazo na kuona nini kinaweza kufanyika. Baada ya kujadili kwa upana wake, tumeona hatuwezi kubariki masuala haya ya kipumbavu, kwa kushiriki katika uchaguzi ambao demokrasia imebakwa.

“Tunataka kuwaambia umma pamoja na Rais John Magufuli, kwamba sisi hatuwezi kubariki uchaguzi na tunatangaza hata viongozi watakaochaguliwa hatutawatambua nchi nzima na tunasema kuwa tutaendelea na vikao na tutaona nini cha kufanya.”

Ameongeza: “Hatuwezi kuwalaumu watendaji kwa kuwafanyia mizengwe wagombea wetu. Hatuamini kama watendaji wanaweza kufanya figusi hizo  rais asijue, waziri mkuu asijue, wala Jafo (Sulemani Jafo, waziri wa Tamisemi), asijue. Hii ni hujuma na haingii akilini, kwamba haikupangwa na wakubwa.”

Haikuweza kufahamika mara moja, iwapo msimamo wa Chadema wa kujiondoa kwenye uchaguzi huo, utaungwa mkono na vyama vingine vya upinzani, hasa chama kinachokuwa kwa kasi nchini cha ACT- Wazalendo.

MwanaHALISI ONLINE lilimuuliza mkurugenzi wa uenezi wa chama hicho, Addo Shaibu, ili kufahamu iwapo chama chake, kitaungana na Chadema, lakini aligoma kuzungumzia suala hilo kwa sasa.

Alisema, “ni kweli kwamba uchaguzi huu, umevurugwa kwa makusudi na serikali ya CCM. Lakini chama ni vikao. Nasi tutakutana na kutoa msimamo wetu. Kwa sasa, naomba niseme, viachwe vikao vya chama, vifanye maamuzi.” 

Vyama vya upinzani nchini vimekuwa vikidai kufanyiwa mchezo mchafu katika mchakato wa uchaguzi huo, ikiwamo madai kuwa wagombea wake, kubughudhiwa katika mchakato wa kuchukua fomu, kurejesha na uteuzi.

Katika kukabiliana na tatizo hilo, Chadema kiliwasilisha malalamiko yake kwenda ofisi tofauti, ikiwamo ofisi ya waziri mkuu, kulalamikia ukiukwaji wa kanuni unaosema unafanywa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.

Nakala za barua hiyo, zimewasilishwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, ofisi ya Rais (Tamisemi) na ofisi mbalimbali za mabalozi.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, hatua ya Chadema na pengine vyama vingine kujiondoa katika uchaguzi huo, litakuwa pigo kubwa kwa serikali ya Rais John Magufuli.

“Hii serikali inatuhumiwa na jumuiya ya kimataifa kuminya demokrasia. Hatua yake ya kuvuruga uchaguzi huu na uamuzi wa upinzani kususia  uchaguzi, hakuna shaka kuwa litakuwa pigo kubwa kwa Rais Magufuli na chama chake,” ameeleza mmoja wa wabunge wa chama tawala ambaye hakupenda kutajwa.

Taarifa zinasema, hatua ya serikali kuamua kuvuruga uchaguzi huo, imetokan ana hofu ya kushindwa kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo, kile kinachoitwa, “wananchi wana njaa inayotokana na uchumi mbaya sana.”

Kingine kinachotajwa kuwa kimesababisha kuvurugwa kwa uchaguzi huo, kunatokana na CCM kukumbwa na mgawanyiko unaotokana na kura za maoni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

20 wafariki dunia kwa mafuriko Manyara

Spread the loveMVUA za vuli zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimeleta madhara...

Habari za Siasa

Dk. Biteko aagiza wakurugenzi TANESCO kukemea rushwa kwenye maeneo yao

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the loveKWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the loveRAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote...

error: Content is protected !!