July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema wamuomba Rais Samia amfutie mashtaka ya ugaidi Mbowe

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, amuagize Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, amuondolee mashtaka ya ugaidi Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ili aendelee na majukumu yake ya chama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa leo Jumamosi, tarehe 31 Julai 2021 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akizungumza na wanahabari mkoani Dar es Salaam, kuhusu maazimio ya vikao vya Kamati Kuu ya chama hicho, vilivyofanyika hivi karibuni.

“Chama kinamtaka Rais Samia, kupitia kwa DPP kuliondoa shauri hili mahakamani na Mbowe awe huru kutekeleza majukumu yake,” amesema Mnyika.

Mnyika, ameziomba jumuiya za kimataifa, ziingilie kati sakata hilo ili Mbowe aachwe huru.

“Kwa kuhakikisha Mbowe anakuwa huru, namna pekee kufanya hivi ni kwa pamoja Watanzania wote na jamii ya kitaifa na kimataifa, kuungana kuitaka Serikali ya Rais Samia iondoe mashtaka haya,” amesema Mnyika.

Rais Samia Suluhu Hassan

Mbowe aliyeko rumande katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam alikamatwa akiwa katika Hoteli ya Kingodom Mwanza, usiku wa kuamkia tarehe 21 Julai, 2021, akijiandaa kushiriki kongamano la kudai katiba mpya, lililoandaliwa na Chadema.

Baada ya kukamatwa Mwanza, Mbowe alipelekwa katika Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alikohojiwa dhidi ya tuhuma za ugaidi zinazomkabili.

Mbowe alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Julai 2021 na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na ugaidi.

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema

Kwa mujibu wa mashtaka hayo, Mbowe anadaiwa kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi. Inadaiwa kuwa, Mbowe alitenda makosa hayo kati ya Mei na Agosti, 2020, kwenye Hoteli ya Aishi, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kesi ya Mbowe, inatarajiwa kusikilizwa tena tarehe 5 Agosti, 2021, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha nyaraka muhimu katika Mahakama Kuu, kwa ajili kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

error: Content is protected !!