Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema wamtunishia misuli Jaji Mutungi
Habari za SiasaTangulizi

Chadema wamtunishia misuli Jaji Mutungi

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
Spread the love

SAKATA la wabunge wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuvuliwa uanachama wa chama hicho, sasa limechukua sura mpya. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua ya sakata hilo kuchukua sura mpya inatokana na hatua ya Chadema kumgeuzia kibao Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa kumtaka kuacha kuingilia michakato ya kinidhamu, inayotekelezwa ndani ya chama hicho.

Chadema kupitia mkutano wake wa Kamati Kuu (CC), uliofanyika tarehe 9 na 10 Mei mwaka huu, iliamua kuwavua uanachama wabunge wake wanne kwa madai ya “kukiuka maadili na utovu wa nidhamu.”

Wabunge waliovuliwa uwanachama, ni pamoja na Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini); Anthony Komu (Moshi Vijijini); David Silinde (Momba) na Joseph Selasini (Rombo).

Akizungumza na waandishi wa habari, siku 10 zilizopita, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema, wabunge hao wamefukuzwa uanachama na kwa kosa la kukaidi agizo la kutaka wasiingie bungeni kwa siku 14 ili kujikinga na Corona (Covid 19).

Aidha, Mnyika alisema, wabunge hao wamefukuzwa kutokana na kutoa kauli za kejeli dhidi ya viongozi wa Chadema, walipotakiwa kutohudhuria vikao vya Bunge kuanzia Tarehe 1 hadi 17 Mei 2020.

John Mnyika, Karibu Mkuu wa Chadema

Akizungumza na MwanaHALISI ONLINE, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Itifaki wa Chadema, John Mrema amesema, “msajili hana mamlaka ya kutupangia la kufanya ndani ya chama chetu.”

Hatua ya Chadema kumtaka Jaji Mutungi kujiweka kando na chama chao, imetokana na uamuzi wa msajili huyo, kukiandikia barua Chadema, akikitaka kujieleza juu ya uamuzi wake wa kuwafukuza uanachama wabunge wake.

Jaji Mutungi amechukua uamuzi huo, baada ya wabunge hao kumwandikia barua, akimtaka aingilie kati, kwa maelezo kwamba walifukuzwa kinyume cha sheria na katiba ya Chadema.

Madai mengine yanayoelezwa na wabunge hao, ni kutopewa haki ya kujitetea dhidi ya tuhuma zao; mwenyekiti wa chama Freeman Mbowe, kuwa ndiye mlalamikaji, mwendesha mashitaka na jaji katika shauri hilo.

Mrema amesema katika barua yao ya majibu kwa Jaji Mutungi, Chadema ilimweleza wazi kuwa ofisi yake, haina mamlaka ya kuingilia michakato ya ndani ya vyama.

“Ni kweli kwamba Msajili ametuandikia barua akisema, ‘amepokea malalamiko kutoka kwa wabunge ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu. Na tayari tulishamjibu, kwamba hana mamlaka ya kutupangia cha kufanya,” ameeleza Mrema.

Amesema, “barua yake ilikuja wiki iliyopita na tulimjibu tangu juzi Jumatatu. Kwenye  majibu yetu tumemueleza wazi kwamba, kwa mujibu wa sheria, kifungu alichonukuu hana mamlaka ya kuingilia michakato ya kinidhamu ndani ya vyama.”

Mrema amewataka wabunge waliofukuzwa uanachama, kukata rufaa dhidi ya hatua hiyo ndani ya Chadema, na kama wakishindwa, waende mahakamani wakiupinge uamuzi huo.

Ameongeza: “Kama hao wabunge wanataka kukata rufaa, wafuate michakato ya kikatiba ya ndani ya chama au waende mahakamani wakatafute suluhisho kama wanataka kufanya hivyo. Lakini sio Msajili kuingilia mchakato.”

Mrema amesema kwa sasa Chadema inasubiri majibu kutoka kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, juu ya suala hilo.

Hata hivyo, wakati Mrema anasema wabunge wake wanaruhusiwa kwenda mahakamani kupinga kufukuzwa uwanachama, Katiba ya Chadema, inapiga marufuku mwanachama wake wa ngazi yoyote kupeleka masuala ya chama mahakamani.

Kwa mujibu wa katiba hiyo, mwanachama au kiongozi anayepeleka masuala ya chama mahakamani, ikiwamo kupinga maamuzi ya vikao vya chama, anakuwa amejifukuza uwanachama.

Mbali na wabunge hao kumwandikia barua ya malalamiko Jaji Mutungi, Mnamo tarehe 11 Mei 2020, Spika wa Bunge Job Ndugai, akiwa bungeni jijini Dodoma, alimtaka msajili huyo kuingilia kati sakata hilo.

Spika Ndugai alisema bado anawatambua wabunge hao na kuwataka waendelea kushiriki shughuli za bunge,  kwa kuwa hawajafanya kosa lolote.

“Wabunge mnaapishwa na spika na karibu wote nimewaapisha mimi mwenyewe, sasa wala msiwe na wasi wasi. Hakuna cha nini wala nini, vikao vya majungu havifanyi kazi. Msjaili hebu aangalie vyama vya namna hii, atazame vyama vya namna hii,” alisema Spika Ndugai.

MwanaHALISI lilipotaka maoni yake kuhusiana na majibu hayo ya Chadema, Jaji Mutungi alieleza kuwa ofisi yake inaendelea kushughulikia malalamiko hayo, kisha atatoa majibu pindi mchakato huo utakapokamilika.

“Tuko kwenye mchakato, tukimaliza tutawafahamisha,” ameeleza Jaji Mutungi.

Alitoa kauli hiyo, leo Jumatano katika mahojiano yake kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi.

Kwa mujibu wa sheria mpya ya vyama vya siasa, Msajili ana mamlaka ya kuingilia michakato ya uchaguzi ndani ya vyama na maamuzi ya kinidhamu yanayochukuliwa dhidi ya wanachama na viongozi wake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

error: Content is protected !!