January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yaridhia Dk. Slaa kupumzika

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) akiwa na Katibu wake, Wiibrod Slaa

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekubaliana na Dk. Willibroad Slaa, katibu mkuu wa chama hicho, kumpumzika kwa muda ili kujitafakari. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

“Chama kimekubaliana na Dk. Slaa kwamba wakati anamalizia shughuli zake, mchakato wa uchaguzi uendelee. Ataukuta mbele ya safari,” ameeleza Freeman Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa Chadema.

Amesema, “…tumekubaliana aendelee na pumziko lake. Akimaliza tutaungana naye tutakapokuwa.”

Mbowe, alikuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa (BKT) la chama chake, jijini Dar es Salaam, leo mchana.

Alikuwa anatoa taarifa kwa baraza kuu sababu za kutokuwapo kwa Dk. Slaa. Alisema, hatua ya mwanasiasa huyo kuomba kupumzika inatokana na ujio wa Edward Lowassa ndani ya Chadema.

“Nimezungumza na Dk. Slaa kwa saa kadhaa jana, lakini hatukufikia mwafaka. Baadhi ya wajumbe wa kamati kuu (CC), nao wamezungumza naye. Lakini wote amewaambia kuwa anaomba muda apumzike; na sisi hatuna shida na ombi lake,” ameeleza Mbowe.

Akizungumza kwa undani suala hilo, Mbowe alisema, Dk. Slaa alishiriki hatua zote muhimu zilizopitiwa kabla ya Lowassa kujiunga na Chadema; alibadilika ghafla wakati wa mkutano wa Kamati Kuu (CC).

Akizungumza kwa kujiamini, Mbowe amesema, chama hakiwezi kusimama kufaya shughuli zake kusubiri maamuzi ya mtu mmoja. Sisi tunaendelea na shughuli zetu hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

“…leo nimeamua kuliweka wazi suala hili baada ya kusikia na kuona vyombo vya habari mbalimbali vikiripoti habari zisizo za kweli kuhusu Dk. Slaa. Wameandika Dk. (Slaa) amejiuzu na chama kimepora mali zake na kumtishia. Napenda kuwahikishia kuwa habari hizo siyo za kweli na wala chama hakina ugomvi naye,” ameeleza Mbowe.

Amesema, Chadema kipo tayari kumpokea Dk. Slaa wakati wowote atakapokuwa tayari kurudi katika nafasi yake.

Aidha, Mbowe amewataka wanachama na viongozi wa Chadema kuondoa hofu kutokana na ujio wa Lowassa ndani ya chama chao kwa kile alichoeleza, “chama kiko salama na kinaheshimu mchango wa kila mmoja.”

Alisema, “ujio wa Lowassa ndani ya Chadema umewajaza watu wengi hofu. Chama chenu ni makini na kitaendelea kuwa makini katika kusimamia maslahi ya taifa.”

Akizungumza na waandishi kabla ya kuanza mkutano wa Baraza Kuu, Mbowe alisema, kulifanyika vikao vingi vya majadiliano juu ya ujio wa Lowassa katika Chadema na yote yaliyofikiwa ni makubaliano ya viongozi, Dk. Slaa akiwamo.

Amesema, wanachama hawatakiwi kuhofia chochote juu ya ujio wa Lowassa na wafuasi wake kwani Chadema ni chama cha wananchi kwa yoyote atakae hitaji kujiunga anakaribishwa.

Amesema, “Lakini hofu hii haipo kwetu tu ipo hata kwao Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani hawajawahi kupata hofu na viboko kama hivi vya kuondokewa na wafuasi wengi tena kwa wakati mmoja.”

Amesema, chama tawala bado hakijielewi baada ya kupata mapigo yaliyotokana na kuondoka kwa Lowassa. Ameahidi kuwa kuna kundi kubwa la wanachama na viongozi wa CCM watakaojiunga na Chadema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.

“Naomba tuitumie fursa hii tuliyoipata kuibomoa CCM. Tumeshawapokea wengi na tuzidi kuwapokea wengine,” ameeleza Mbowe.

Mkutano mkuu wa Chadema unatarajiwa kufanyika kesho katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Lowassa anatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa mgombea urais, kupitia muungano wa UKAWA.

Naye Juma Duni Haji, mwanachama na kiongozi kutoka Chama cha Wananchi (CUF), anatarajiwa kutangazwa kuwa mgombea wake mwenza.

error: Content is protected !!