June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema wamgomea Rais Samia, wamtaka aunde tume kusaka katiba mpya

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

CHAMA kikuu cha upinzani nchini Tanzania- Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekataa ombi la Rais wa Taifa hilo, Samia Suluhu Hassan la kutaka apewe muda kwa ajili ya kufufua mchakato wa katiba na kuondoa zuio la mikutano ya hadhara. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Chadema kimesema, hakitapiga magoti kuomba katiba na kitaidai asubuhi, mchana na jioni bila kuchoka hadi ipatikane.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, tarehe 1 Julai 2021 na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati akifungua kongamano la kudai Katiba Mpya, lililofanyika katika ukumbi wa Baracuda, Tabata jijini Dar es Salaam.Kongamano hilo, limeandaliwa na Baraza la Vijana Chadema (Bavicha).

“Kwanza tuna amani mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni haki ya kikatiba, kisheria na ni wajibu wetu, ombi la Mama Samia kwamba tusubiri, tumpe muda hatuko tayari kumpa muda,” amesema Mbowe

“Hatuko tayari kumpa Mama Samia muda, na natoa agizo kwa viongozi wote wa chama nchi nzima, wajiandae mapema kwa ajili ya mikutano ya hadhara, siku ambsyo tutaitangaza,” amesema Mbowe.

Jumatatu iliyopita ya tarehe 28 Juni 2021, Rais Samia akizungumza na wahariri na waandishi wa habari, Ikulu ya Dar es Salaam, kuhusu siku 100 za utawala wake, alisema suala la katiba mpya na mikutano ya hadhara, ni ya muhimu lakini kwa sasa aachiwe aisimamishe nchi kiuchumi.

Kuhusu mikutano ya hadhara, Mbowe amesema, wabunge walioruhusiwa kufanya mikutano hiyo hawajachaguliwa kihalali na wananchi.

“Mama anasema wabunge wanafanya mikutano kwenye maeneo yao mambo aliyosema mwendazake, tuna mkumbusha Rais Samia hao wabunge na madiwani unaosema wafanye mikutano kwenye maeneo yao hawakuchaguliwa na wananchi wa Tanzania.”

“Kama zaidi ya nusu ya wabunge wameingia bungeni kwa mlango wa uani, leo wanahalalishwa wanapewa amri ya kufanya mikutano wale walioibiwa wanazuiwa kungojea kibali cha mama. hatusubiri kibali cha mama,” amesema Mbowe.

Mwenyekiti huyo wa Chadema amesema, Tanzania inahitaji Katiba mpya ili kuimarisha utawala wa sheria na utawala bora pamoja na uchumi.

“Tunataka katiba mpya itakayofanya Watanganyika na Wazanzibar wakae pamoja kwa mapenzi na si kwa kulazimishwa na utawala. Katiba ambayo itahakikisha haki inapatikana kwa wote. Katiba itakayojenga taasisi imara na kudhibiti viongozi wanaotumikia vibaya madarama yao, katiba itakayoleta muafaka wa kitaiafa,” amesema Mbowe.

Wakati huo huo, Mbowe amemuomba Rais Samia, aunde Tume ya Katiba, itakayoshirikisha makundi yote kwa ajili ya kufufua mchakato wa katiba mpya.

“Hatua ya kwanza mama aunde tume ya katiba na tume hiyo isiwe ni tume ya chama chake, wala isiwe ni tume ya Chadema peke yake. Iwe tume shirikishi itakayotambua makundi maalum katika jamii, ikiwemo viongozi wa kiroho, waislamu na wakristo.”

“Makundi mengine muhimu yakiwemo yasiyo ya kiserikali, vyama vya siasa. Taasisi za kitaaluma wasomi wetu, makundi ya wafanyabishara, wakulima, sio bunge zima bali kamati ambayo hatutegemei itazidi wajumbe 15,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema baada ya tume hiyo kuundwa, bunge la katiba liundwe kwa ajili ya kukamlisha zoezi hilo.

“Pili, kamati ichukue rejea ya mapendekezo ya Jaji Joseph Warioba halafu ikaangalie katiba iliyopendekezwa na wabunge wa CCM, kuona tulitofautiana wapi na katiba ya Warioba.”

Rais wa Tanzania,
Samia Suluhu Hassa

“Mbali ya kupata bunge la katiba, hii ipunguze tofauti za makundi, hatimaye hatua ya pili iundwe bunge ambayo itapelekewa rasimu ya katiba ambayo imeshaangalia maslahi ya makundi mbalimbali badala ya maslahi ya chama kimoja cha siasa,” amesema Mbowe

“Lisiwe bunge la muundo kama lile lililoleta mgogoro, wasifikiri bunge hili walilochakachua litaunda katiba ya wananchi, hatutaelewana.”

Kwa sasa nchini Tanzania, wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu wameufufua upya mjadala wa mchakato wa Katiba Mpya, uliositishwa Aprili 2015, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa.

NEC ilisitisha hatua hiyo ya mwisho ya upatikanaji Katiba Mpya, kutokana na zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura kutokamilika kwa sababu ya hitilafu zilizojitokeza katika mshine za BVR.

Tangu zoezi hilo kusitishwa chini ya aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, halikuendelea tena katika awamu zilizofuata.

Aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli, aliweka kando mchakato huo kwa maelezo kwamba alitaka kuijenga nchi.

error: Content is protected !!