June 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema wala kiapo

Spread the love

SIKU moja baada ya mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuzuiwa, chama hicho kimeapa kutofuata ‘upuuzi’ wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Happiness Lidwino.

“Lengo la Serikali ya CCM halitatimia kwani hatuwezi kuufuata upuuzi wao bali tunakaa kimya kwa muda ambapo kama chama tuna mpango wa kukutana  kesho kwenye kikao,” amesema Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar akizungumzia hatua ya kuzuiwa mikutano yao ya hadhara.

Mwalimu amesema, Serikali ya CCM inajaribu kuwachokoza mchana kweupe ili wapate hasira na wachukue amuzi mgumu utakaoingiza nchi mahali pabaya.

“Kwa kuwa wameonesha uoga na kujihami hatutafanya hivyo, tutatumia busara kuchukua maamuzi,” amesema Mwalimu.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii na kueleza kuwa, tukio lililotokea jana mkoani Shinyanga, Kahama kwa Jeshi la Polisi kuvamia mkutano na kuusambaratisha ni, kukichokonoa chama hicho ili kichukue uamuzi mgumu.

“Hatutafanya mikutano tena hadi pale tutakapotoa tamko na maamuzi ya kama tutaendelea na mikutano au tutasitisha,” amesema Mwalimu.

Hata hivyo, Mwalimu ameeleza kuwa, CCM ina mpango wa kukifilisi chama hicho kwa kuwa taarifa ilipelekwa polisi na kibali cha kufanya mikutano kilitoka.

Na kwamba waligeukwa na kuvamia mkutano huo huku maandalizi yakiwa yamekamilika, “chama kimepata hasara kubwa.”

Amesema, “kutokana na tukio hilo la uvamizi, wananchi kadhaa walijeruhiwa, upotevu wa mali za wananchi huku baadi ya viongozi na wananchama 32 walikamatwa na polisi na leo wamefikishwa mahakamani huko Kahama.”

Jana vurugu kubwa zimetokea baina ya Jeshi la Polisi na wananchi kwenye mkutano wa chama hicho na kusababisha sintofahamu.

Jeshi la Polisi lilitumia maji ya kuwasha pamoja na mabomu ya machozi kutawanya watu waliokuwepo kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Chadema mjini Kahama.

Mkutano huo ulikuwa ni uzinduzi wa ‘Dai Demokrasia’ ambapo Jeshi la Polisi liliingilia kati na kuuzuia ikiwa ni muda mchache baada ya Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa nchini.

Hata hivyo, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa alisema kuwa, pamoja na vitisho vya demokarsia nchini, chama hicho hakitarudi nyuma kudai haki.

Mbowe alisema kuwa, wataendelea kudai haki ya demokrasia nchini ndani ya mahakamani, bungeni, ndani na nje ya nchi.

error: Content is protected !!