Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema wahoji alipo Rais Magufuli, Majaliwa awajibu
Habari za SiasaTangulizi

Chadema wahoji alipo Rais Magufuli, Majaliwa awajibu

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema
Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Mandeleo (Chadema), kimeitaka serikali ya Tanzania kuvuja ukimya juu ya mahali alipo Rais John Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam  … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, tarehe 12 Machi 2021, katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika, ametaka umma uelezwe mahali ambako “rais yupo na hali yake ya kifya ikoje.”

Kwa mujibu wa Mnyika, ni muhimu maswali hayo mawili yakajibiwa, ili kuondoa uvumi unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ukidai “Rais Magufuli, ni mgonjwa.”

Mnyika amesema, jana Alhamisi, viongozi wakuu wa Chadema, wakiongozwa na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho taifa, walikutana kwa njia ya mtandao, kujadili mambo mbalimbali ya kisiasa, yanayohusu nchi.

Miongoni mwa yaliyojadiliwa, ni pamoja na “sintofahamu inayoendelea mitandaoni na kwenye vyombo vya habari vya kimataifa, vikihoji ni wapi alipo Rais Magufuli, na yuko kwenye hali gani.”

Amesema, “baada ya kumaliza kikao hicho, tumekubaliana nije mbele yenu waandishi kutoa maazimio ya kikao hicho. Tumekubaliana kuitaka serikali kuvunja ukimya na kujitokeza hadharani iseme yuko wapi Rais Magufuli na yuko kwenye hali gani.”

Mnyika amedai kuwa “mara ya mwisho Rais Magufuli kuonekana hadharani, ilikuwa tarehe 27 Februari 2021.”

Amesema, muda huo wa karibu wiki mbili sasa, ni mrefu na niwajibu wa wananchi kupata haki yao na kila mtu anayo haki kupata taarifa kama inavyoelezwa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Mtendaji huyo mkuu wa Chadema amesema, kauli zilizotolewa watu mbalimbali wakiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba hazijajibu maswali mawili muhimu: “Rais yuko wapi na ana hali gani?”

Huku Mnyika akitaka wananchi waelezwe na mamlaka sahihi za serikali, mahali aliko Rais Magufuli, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema, kiongozi huyo mkuu wa nchi, anaendelea kuchapa kazi.

Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati anazungumza baada ya kushiriki katika Sala ya Iijumaa kwenye Msikiti wa Ijumaa, Njombe mjini.

Majaliwa amewataka Watanzania hususan walioko nje ya nchi hiyo, kuwapuuza kwa kueneza uzushi unaoweza kuleta taharuki usiokuwa na tija kwa Taifa lao kwani hawapendi maendeleo ya nchi na wanatamani kuona Taifa likiporomoka.

”…tuwapuuze baadhi ya Watanzania ambao wamejawa na chuki tu, wamejawa na husda tu na wanatamani kuwachonganisha na kutaka kushuhudua Taifa hili likiporomoka.

”Kuanzia juzi hata leo asubuhi, nimeona Watanzania wenzetu wenye husda tena hawako ndani wako huko wanashawishi vyombo vya Kimataifa viseme Rais wa Tanzania anaumwa kajifungia hizo ni chuki tu, husda tu,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema ”Watanzania tulieni uongozi wenu upo imara na mafanikio tunayaona, kumzushia rais ugonjwa ni chuki, wanasema atoke aende wapi? Ulishamkuta siku moja anazurura Kariakoo? Rais anampango wake wa kazi si mtu wa kuzurura.”

Waziri Mkuu amesema, Rais Magufuli anawasaidizi wake kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijijini na kwamba anafanyakazi kulingana na mpangokazi wake, hivyo amewataka Watanzania waendelee kuwa na amani huku wakiamini Serikali yao.

Awali, leo asubuhi, mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila alisema, amefanya mazungumzo na Rais Magufuli, anayeendelea na kuchapa kazi.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Albert Chalamika

Amesema, “leo asubuhi, nimempigia simu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (John Magufuli), kumshukuru kwa fedha alizotupa za kutekeleza miradi ya maendeleo na kwa kweli amenijibu kwa furaha na faraja kubwa mno.”

Katika kusisitiza hilo, Chalamila amesema, “hao wanaozungumza rais yuko kwenye matibabu labda wao wako kwenye matibabu. Kwa kweli, Dk. John Pombe Magufuli, he is very strong (yupo imara) na anaendelea kufanya kazi zake vizuri sana.”

Kauli ya Majaliwa, Chalamila, imekuja katika kipindi ambacho viongozi mbalimbali, akiwamo Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba, wamekuwa wakijaribu kujibu uvumi uliokuwa ukionezwa mitandaoni na watu kadhaa akiwemo makamu mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu, kwamba Rais Magufuli ni mgonjwa na amelazwa kwenye hopitali moja jijini Nairobi, nchini Kenya.

Hata hivyo, Lissu hajataja vyanzo vyake vya taarifa na hajaweza kuthibitisha kwa uhakika, kuwa Rais Magufuli, yuko nchi gani.

Mwigulu Nchemba

Badala yake, mwanasiasa huyo anayeishi nchini Ubelgiji kwa sasa, aliishia kung’ang’aniza kuwa “Rais Magufuli, ni mgonjwa na amelezwa Nairobi” na baadaye kuongeza, “mara ya mwisho Rais Magufuli alionekana hadharani, ilikuwa tarehe 27 Februari 2021.”

Akimjibu Lissu, Mwigulu amesema: Kiongozi wa nchi sio Parish Worker kanisani; wala sio Mzee wa Kanisa kwamba alipangiwa zamu na hakuonekana.”

Amesema, “kiongozi wa nchi sio mtangazaji wa TV kwamba alikuwa na kipindi ila hakuonekana, kiongozi wa nchi sio kiongozi wa jogging clubs kwamba anatakiwa kuwa tu mtaani kila siku na kurusha selfie.

“Tuache upuuzi upuuzi hata kama hatuna jambo la kufanya, umeichafua sana nchi umeshindwa, mmetamani tukwame mmeshindwa, sasa mnaombea mabaya nchi yetu na kiongozi wa nchi yetu, sheria inapovunjwa hakuna mipaka wala hakuna muda kupita, kwa wanaoropoka zingatieni kifungu cha 89 cha Penal code na 16 cha Cyber Crime, Serikali ipo kazini.”

Innocent Bashungwa, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Naye Bashungwa, alitoa wito kwa waandishi wa habari na wananchi, “kuendelea na utaratibu wa kupata taarifa kupitia vyanzo rasmi vya habari, kutumia uvumi kama habari rasmi ni kukiuka sheria zinazosimamia sekta ya habari, epukeni kusambaza habari ambazo mtawajibika nazo.”

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM), Hamis Taletale maarufu ‘Babu Tale’ jana Alhamisi, alitumia ukurasa wake wa Instagram kuzungumzia ‘uzushi’ huo dhidi ya Rais Magufuli.

Andishi la Babu Tale ambaye pia ni meneja wa msaani Diamond Platinum lilisoma: “Nawashangaa sana wanaosambaza uvumi usio na utu, heshima na nidhamu dhidi ya kiongozi mkuu wa nchi yetu. Eti kwa nini hakuonekana kwenye Ibada Jumapili iliyopita, kwani Mhe. Rais huwa anaonekana kila Jumapili?

Hamisi Taletale ‘Babu Tale’

“Mimi ni Mtanzania ninayefuatilia taarifa za Rais wangu bila kukosa, sio Jumapili zote hutolewa taarifa za Rais kuhudhuria Ibada.”

Anasema, ameshangazwa pia na hatua ya nchi jirani kuingia kichwakichwa, kuwa Rais kaenda kutibiwa maradhi ya moyo na Korona Nairobi.

Babu Tale anahoji: “Hivi kama Rais anatafuta rufaa, ndio apelekwe Nairobi? Yaani Rais aache kwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo ni moja ya vituo bora Afrika kwa kutibu maradhi ya moyo aende Nairobi? Wakati Wakenya kibao wanakuja kutibiwa Moyo Tanzania. Acheni hizo.

“Mhe. Rais wewe chapa kazi, hawa tutajibizana nao sisi, wewe wala usihangaike nao, wala serikali msihangaike nao. Bahati nzuri wanaoendesha ajenda hii ni Watanzania wenzetu na tunawajua, na tunajua sasa hivi hawana hoja wamebaki kusingizia watu kufa na kubangaiza hoja kupitia ugonjwa wa Korona.

“Tunaendelea kukuombea Rais wetu, Mungu akupe afya njema, busara na hekima ya kuendelea kuliongoza Taifa letu.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

M/kiti bodi ya wadhamini Chadema afariki dunia

Spread the loveMWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Zitto: Nikifa Ado atavaa viatu vyangu

Spread the love  KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe...

error: Content is protected !!