March 2, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema waanika ubatili wa NEC kwenye uchaguzi wa marudio

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

KUHUSU NEC KUHALALISHA UBATILI ULIOFANYIKA KWENYE UCHAGUZI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeshtushwa na kiwango cha uongo na upotoshaji unaooneshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hali ambayo inadhihirisha kuendelea kuhalalisha vitendo vya kuharibu na kuvuruga uchaguzi vilivyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa marudio uliofanyika Agosti 12, mwaka huu.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana ikilenga kujibu mojawapo ya nchi wahisani wa maendeleo nchini ambayo ilitoa tamko la kuonesha kuguswa na matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi huo, NEC wameamua kutaka kuidanganya jamii ya Watanzania, Jumuiya ya Kimataifa na hata dunia nzima kwa ujumla kuhusu kilichotokea kwenye mchakato wa uchaguzi uliohitimishwa Agosti 12, mwaka huu.

1. Jamii ya Watanzania, Jumuiya ya Kimataifa na Dunia nzima iliona na kushuhudia kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari ikiwemo vyombo vya habari (mainstream na online social media) jinsi ambavyo NEC ilishindwa kabisa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki, kutokana na ama kutokuwa na uwezo au kufumbia kwa makusudi hila na njama zilizokuwa zikifanyika kuharibu na kuvuruga uchaguzi huo.

2. Njama hizo zilianza tangu mapema, mathalani Wagombea udiwani wa CHADEMA katika kata tano kule Tunduma walinyimwa fomu zao za kugombea kwa makusudi kabisa kisha fomu hizo wakapewa watu wengine (wanaodaiwa hawajulikani) kwa kutumia mbinu za kijinai zinazohusisha kughushi. Kama hiyo haitoshi wagombea wetu wakaanza kusakwa na kukamatwa na polisi na kubambikiwa tuhuma za jinai.

3. Tumesikitishwa na taarifa hiyo ya NEC kuhoji maswali kadhaa ambayo yanazidi kuonesha uzembe wa taasisi hiyo kubwa au kushiriki kuhalalisha ubatili. Mathalani wameihoji nchi hiyo ilitumia utaratibu gani kupata taarifa ilizotoa kuwa uchaguzi uligubikwa na vitendo vya vurugu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi! Swali hilo la NEC linabua swali jingine, je mamlaka zilizoharibu na kuvuruga uchaguzi huo zilifanya hivyo kwa sababu zilijua hakuna waangalizi wa kimataifa? Je zilifanya hivyo kwa sababu zilijua habari za matukio hayo hazitaufikia ulimwengu ambao hautakaa kimya?

4. Hivi NEC walitarajia matukio kama ya kuzuia mikutano ya kampeni za uchaguzi ya CHADEMA kinyume kabisa na sheria za nchi na taratibu za uchaguzi, kupigwa, kujeruhiwa na kukamatwa kinyume cha sheria kwa wabunge, viongozi wa Chama na waandishi wa habari waliokuwa kazini (kama ilivyokuwa kule Turwa) vilikuwa havionekani na dunia nzima?

5. Hivi NEC inaamini kuwa ni Watanzania pekee wa Arusha walioshuhudia na kujionea mgombea wa CHADEMA akipigwa, kujeruhiwa na kunyang’anywa fomu yake ya kugombea kwenye Ofisi ya Serikali, mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi kisha akanyimwa fomu zingine na hivyo kupoteza haki yake ya kugombea?

6. Je NEC wanaamini kuwa vitendo vya kuwazuia au kuwaondoa mawakala wa CHADEMA kwenye vituo vya kupigia kura kinyume na taratibu za uchaguzi vingebakia kuwa siri ya watekelezaji wa vitendo hivyo? Je NEC inafikiri kuwa vurugu walizofanyiwa wagombea na mawakala wa CHADEMA wakiwa vituoni, ikiwemo kupigwa, kujeruhiwa, kuondolewa na kubambikiwa kesi visingejulikana duniani kote? Au kuwanyima fomu za matokeo na kubadili matokeo halisi (mathalani Buyungu) ingebakia kuwa siri yao? Au kuwaondoa kwa hila wagombea wa CHADEMA huku tume ikibariki kwa kukataa kusikiliza rufaa wala kuitisha kikao cha Kamati ya Maadili ya Taifa ni siri ya ndani ya nchi?

Tunaikumbusha NEC kutambua kuwa uchaguzi si tukio la siku moja, bali ni mchakato, kwa kuzingatia hilo CHADEMA ikiwa kama mdau mkubwa wa uchaguzi, ilijitokeza tangu mwanzo kuelezea namna ambavyo kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Uchaguzi na kanuni zake hali ambayo ilikuwa ni dalili ya kuwepo kwa mipango na hujuma za kuvuruga na kuharibu uchaguzi hivyo kutokuwa huru na haki.

Ni aibu kubwa na dalili mbaya kwa mwenendo wa misingi ya utawala bora kwa nchi yetu, kujaribu kuwahadaa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa kilichofanyika katika uchaguzi wa marudio wa Agosti 12 na zingine kabla ya hapo kuwa ni uchaguzi huru na haki.

Ni kweli kuwa Tanzania ni nchi huru, lakini uhuru huo unaenda sambamba na wajibu wa kusimamia, kutekeleza na kuendesha masuala yake kwa kuzingatia mambo muhimu kama kulinda haki za binadamu, Katiba ya Nchi na sheria zake, sheria za kimataifa na mikataba mbalimbali ambayo Tanzania imesaini na kukubaliana nayo.

Ni vyema Serikali ya Tanzania kwa ujumla wake na watumishi wa umma waliopewa mamlaka katika vyombo mbalimbali wakatambua kuwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu, sheria na Katiba ya Nchi vinavyofanyika bila hatua yoyote kuchukuliwa dhidi ya wahusika, vinaangaliwa na kufuatiliwa na Jamii ya Watanzania na dunia nzima.

Ndiyo maana mara kadhaa tumekuwa tukiwatahadharisha Watumishi wa Umma wanaokubali ‘kutumika’ au wanaojituma wenyewe kufanya na kutekeleza vitendo hivyo kuwa iko siku watawajibika mbele ya sheria, ama katika vyombo vya ndani au vya kimataifa, wao wenyewe kwa matendo yao. Kwa sababu dunia inafuatilia na inajua.

Baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Chama kinachoendelea jijini Dar es Salaam, CHADEMA itatoa tamko la maazimio ya Chama kuhusu mwenendo mzima wa uchaguzi wa marudio na mwelekeo wake.

Imetolewa leo Alhamis, Agosti 16, 2018 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

error: Content is protected !!