August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema: Sura ya Magufuli ni hii

Spread the love

RAIS John Magufuli anatajwa kuwa mtawala anayeendekeza kisasi cha kiutawala kwa wananchi walioamua kupigia kura vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anaandika Regina Mkonde.

Jana wakati Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi namba mbili alisema, “huwezi ukapeleka chakula kwa mtoto wa jirani” kauli ambayo imeeleza kuwa ya kibaguzi.

Kauli hiyo imetafsiriwa na Ukawa kwamba Rais Magufuli anaonekana kutokuwa tayari kushirikiana na vyama hivyo (jirani) licha ya kuwa ndio walio wengi katika kuwawakilisha wananchi jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo pia imejadiliwa kwa upana kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kuwa na ukakasi uliotoa tafsiri mbalimbali.

Charles Kuyeko, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala amesema, kauli hiyo imelenga kuwaponda viongozi wa upinzani na kwamba, inaleta picha mbaya katika ulimwengu wa demokrasia nchini.

“Kauli yake imelenga kuuponda upinzani, licha ya hayo kampeni zimeisha, hakuwa na sababu ya kuongea kauli hiyo mbele ya wananchi katika shughuli za kitaifa ambazo hazilengi itikadi za kisiasa,” amesema Kuyeko.

Amesema kuwa, huu si wakati wa kujadili tofauti za itikadi za vyama bali ni wakati wa kutatua changamoto za wananchi.

Boniface Jacob, Meya wa Manispaa ya Kinondoni amesema kuwa, hata kama rais ataitekeleza kauli yake, haitaathiri maendeleo ya halmashauri yake kwasababu mapato yake yanakidhi mahitaji yake.

“Kwa upande wangu kauli yake haitaniathiri kwasababu Kinondoni tunajiweza hatutegemei sana msaada kutoka serikali kuu. Kinondoni ina uwezo wa kukusanya mapato ya kiasi cha bilioni 50 kwa mwaka,” amesema Jacob.

Amesema, Kinondoni ina vyanzo vingi vya mapato, ambapo mapato yake yanatosha kutekeleza ahadi zake ikiwemo uboreshaji wa miundombinu na huduma za kijamii.

“Hata kama atajaribu kutuwekea vikwazo ili tushindwe tekeleza ahadi zetu na kuonekana hatufai mbele ya wananchi, hatofanikiwa, tutatekeleza ahadi zetu na wananchi watashuhudia mabadiliko ya uongozi wa UKAWA.

Pia amenukuliwa akisema, “nawapongeza wakazi wa Kinyerezi kwa kunichagulia mbunge anayetoka kwenye chama changu, nawahakikishieni kama kuna changamoto za Jimbo la Segerea nitazipa kipaumbele katika utatuzi wake.”

Licha ya hayo, Magufuli amesema aliamua kumchagua Paulo Makonda aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuwanyamazisha maadui zake.

“Hata Makonda nimemuacha Dar es Salaam ili wabaya wake wamuone akipanda cheo, wenye chuki wajinyonge zaidi,” amenukuliwa Rais Magufuli.

error: Content is protected !!