July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema, Polisi wavutana msiba wa Mawazo

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema pamoja na Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza kupiga marufuku uagaji wa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, lakini uagaji upo pale pale. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganizesheni Chadema Taifa, Benson Kigaira, wakati akizungumza na gazeti hili juu ya agizo la Polisi la kupiga marufuku uagaji wa marehemu Mawazo.

Mawazo ambaye aliuawa kinyama Novemba 14 mwaka huu, katika Kata ya Katoro mkoani Geita na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM, kisha kutelekezwa na kutokomea kusiko julikana.

Kigaira amesema Polisi kwa kushirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kuandaa mipango na mikakati ya uzushi inayoaminisha wananchi kwamba kesho katika uagwaji wa marehemu Mawazo kutakuwepo na vurugu.

Amesema kwamba licha ya polisi kutoa agizo hilo, lakini Chadema kitaendelea na zoezi hilo leo, huku akidai kuwa kama ni suala la vurugu halitakuwepo na kama litatokea litakuwa limepangwa na polisi.

“Tangu jana tuliongea na polisi karibu saa 4, wakawa wanazungumza mambo hayo, kwamba wamefanya uchunguzi wamebaini kutakuwepo na vurugu na uvunjifu wa amani, sasa sisi zoezi hilo lipo pale pale.

“Pia wao wanasema sasa hivi kuna kipindupindu, wanatukataza tusifanye mkusanyiko, mbona hawawatazi kwenye nyumba za ibada na sokoni ambako watu walio wengi ndiko waliko?” amehoji Kigaira.

Mapema leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Mkumbo wakati akizungumza na wanahabari, alipiga marufuku uagaji wa marehemu Mawazo katika mkoa wa Mwanza na kwamba ukaagiwe Geita ambako tukio lilitokea.

“Baada ya timu yetu kufanya uchunguzi na kujilidhisha, tumebaini kuna vurugu zitatokea katika uagaji wa marehemu, hivyo hatutakubali mkusanyiko wowote ule, wakaagie Geita sio hapa Mwanza,” amesema Mkumbo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Onesmo Rwakengera, amesema mpaka sasa katika mkoa wa Mwanza kuna jumla ya wagonjwa 422, wanaotokanana na ugonjwa wa kipindupindu hivyo mikusanyiko isiokuwa ya lazima isifanyike.

error: Content is protected !!