July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema Monduli yapata viongozi wapya

Spread the love

BAADA ya mvutano wa viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliotokea hivi karibuni katika wilaya ya Monduli kwa viongozi hao kuachia ngazi hatimaye chama hicho kimepata viongozi wapya. Anaandika Ferdinand Shayo, Arusha … (endelea).

Akizungumza baada ya kupata viongozi wapya wa chama hicho Mwenyekiti wa Chama Mkoa na Katibu wa Kanda ya Kaskazini Chadema, Amani Golugwa amesema wamefikia hatua hiyo kutokana na nafasi hizo kuwa wazi hivyo waliamua kuziba nafasi hizo kwa kufanya uchaguzi.

Amesema kwamba chama hicho kimewapata Mwenyekiti wa wilaya hiyo Ben Maganga, Erick Godwin ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu taifa, Julius Kalanga ambaye ni Mjumbe wa Kamati Utendaji ya chama Wilaya ya Monduli pia ni mgombea Ubunge jimbo la Monduli.

Golugwa amedai kwamba viongozi walioondoka walikosa uvumilivu wa kisiasa ambapo ilisababisha kutimkia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ameongeza kwamba aliyeondoka ni aliyekuwa mwenyekiti wa jimbo hilo, Sironga Japhet pamoja na Katibu wake lakini kutokana na hali hiyo chama hakikuyumba kiliendelea kuimarika.

Wengine ni ndugu Lekshon katibu wa mwenezi wa chama, Katibu wa chama, Hussein Ole Kunei pamoja na Beni Mganga ambaye atachukua nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama jimbo la Monduli.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa mwenyekiti huyo mpya, Ben Maganga amesema kuwa watahakikisha watashinda kata zote na ngazi ya ubunge kutokana na kujipanga vya kutosha.

Ameongeza kuwa kutokana na suala la uteuzi wa kiongozi kwa ngazi ya ubunge ndio iliyopelekea baadhi ya viongozi kuachia nafasi kwa viongozi waliokuwepo awali kwa kudai kuchezewa rafu.

error: Content is protected !!