July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema mguu sawa! Mbowe  hadi kieleweke

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amewataka viongozi na wafusi wa chama hicho katika ngazi mbalimbali, kutotishika na vitisho vya jeshi la polisi, anaandika Josephat Isango.

Mbowe amewataka wapenzi wa chama hicho wakae mguu sawa kutekeleza maagizo ya Kamati Kuu (CC), iliyoketi jijini Dar es Salaam na kwamba wasitishwe na vitisho vya polisi.

Akizungumza na MwanaHALISI online Mbowe amesema “Kama polisi wataendelea kuniita sababu ya maazimio ya Kamati Kuu niliyosoma mbele ya waandishi wa habari basi wananchi waendelee na maandalizi sababu polisi wamekuwa wakifanya siasa badala ya weledi wa kazi yao.”

18 Septemba mwaka 2014 waliniita baada ya kutangaza maandamano nchi nzima, wakanihoji hawakunikuta na hatia wakaniacha hadi leo hawajawahi kuniita, wanachofanya ni kutupotezea muda wa kufanya siasa kwa mujibu wa sheria, na hilo halikubaliki, aliongeza Mbowe.

2014 Mbowe akiwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) alitangaza maandamano nchi nzima. Kauli hiyo ilisababisha jeshi hilo kumwita Mbowe makao makuu na kisha kumhoji.

Alikuwa akimtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha Bunge Maalumu la Katiba kuendelea kwani ilikuwa ni sawa na kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya, kuiweka nchi rehani, na kufuja fedha za walipakodi,

Katiba hiyo haikupita licha ya fedha lukuki za watanzania kufujwa hadi sasa.

Madai ya sasa ya kumhoji Mbowe kuhusiana na maandamano nchi nzima yalisababishwa na msimamo wa kamati kuu ya chama hicho unaowataka viongozi wa ngazi mbalimbali, wafuasi na wapenzi wa chama hicho kuandamana Septemba 1 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chadema na kutangaza maazimio ya kamati kuu Freeman Mbowe alisema kupitia kikao hicho wamekubaliana kuanzisha operesheni ambayo itafanyika kwa nchi nzima na kuwaagiza viongozi wa wilaya zote nchini wa Chadema kuanza vikao kujiandaa na operesheni hiyo.

“Tumefanya makubaliano ya pamoja na kukubalina kuwa Septemba, 1 tutafanya mikutano nchi nzima na mimi kama mwenyekiti nawaagiza viongozi wa chama wa kila wilaya kuanza kujiandaa na mikutano hiyo,

“Operesheni hii imepewa jina la UKUTA ikiwa na maana ya Umoja wa Kupinga Udikteta nchini sio ili kupinga mtu mmoja kuwa na sauti katika kila jambo na kutaka kuliongoza yeye, hizi ni dalili za udikteta,” alisema Mbowe.

Kamati kuu ya Chadema iliketi kwa dharura Julai 23-26 mwaka huu kwa ajili ya kujadili hali ya siasa na uchumi wa taifa tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani.

Kamati kuu ilitoa taarifa kuwa tangu utawala wa awamu ya tano ulipoingia madarakani mwezi Novemba, 2015 umechukua hatua mbalimbali za kubinya Demokrasia na kuua dhana ya utawala bora kwa njia mbalimbali.

Pia kamati kuu iliainisha makundi ya kijamii ambayo tayari yameshaumizwa au kubinywa na watanzania walio wengi wanakaa kimya kwa sababu wao sio sehemu ya kundi husika ambalo limenyimwa haki au kwa kuwa hajafikiwa moja kwa moja.

Pamoja na mambo mengine, kamati kuu iliweka wazi lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini, kiliyodai kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli.

“Tangu kuanza kwa utawala wa awamu ya tano, kuna matukio mbalimbali ya kubinya demokrasia na kuua dhana ya utawala bora, na yapo makundi ambayo tayari yameshaumizwa, huku Watanzania wengi wakikaa kimya kwa sababu wao si sehemu ya kundi lililominywa.

“Kwa kuwa wewe tayari umeshafikiwa, hauna budi kujenga Ukuta ili kuzuia wengine wasidhurike na utawala huu. Kwa kuwa wewe hujafikiwa na ndiyo maana husemi wenzako wanapofikiwa, basi njoo tujenge Ukuta ili ukifikiwa awepo wa kusema,” alisema Mbowe.

Kutokana na hilo, aliwataka viongozi wa dini zote pamoja na Watanzania wapenda amani, kuungana na chama hicho kujenga Ukuta ili kuzuia uchumi kuporomoka.

“Njoo tujenge Ukuta kuzuia udikteta huu, tujenge Ukuta tuilinde Katiba yetu… Ukuta huu ni wa wananchi wote bila kujali dini, kabila, chama cha siasa au rangi,” alisema Mbowe.

Akizungumzia chimbuko la Ukuta, Mbowe alisema umetokana na Rais Magufuli kupiga marufuku safari zote za nje kwa watumishi wa umma, kuamuru Mahakama Kuu iwahukumu wafanyabiashara ambao wana kesi za kodi ili Serikali ishinde.

Aidha Mbowe alisema sababu zilizowasukuma kuanzisha Ukuta ni pamoja na mabalozi na wanadiplomasia kuzuiliwa kukutana na viongozi wa kisiasa bila kibali cha Serikali, watumishi wa umma kufukuzwa ovyo bila utaratibu kwa kisingizio cha kutumbua majipu bila kufuata sheria na kanuni za utumishi wa umma na mawakili kuunganishwa kwenye kesi za wateja wao wanapokwenda kuwatetea.

Walimu kukatwa mishahara iwapo dawati litavunjika kwenye shule yake, kupotezwa kwa wana-CCM ambao watapinga kauli ya mwenyekiti au kuwa na maoni tofauti, unyanyasaji na udhalilishaji wa viongozi wa dini na wananchi wa Zanzibar ni miongoni mwa sababu alizotaja Mbowe.

“Historia inaonyesha duniani kote hakuna ambako utawala uliwahi kuushinda ukuta wa wananchi, na hii ndiyo nguvu ya umma, kila mmoja achukue hatua popote alipo kujenga Ukuta,” alisema.

Kuhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara Septemba Mosi, Mbowe amesema Kamati Kuu imeagiza ngazi zote za chama kuanzia ya msingi, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda, mabaraza na taifa kukaa na kufanya maandalizi ya mikutano hiyo nchi nzima.

Haya yanajiri ikiwa ni siku kadhaa tangu Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho kutiwa mbaroni kwa madai ya uchochezi

 

error: Content is protected !!