JINA la Tundu Lissu, ndani na nje ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, linakua. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Mwanasiasa huyo nguli wa upinzani nchini, tayari amefunguliwa mlango wa kugombea urais kupitia chama hicho, endapo atakuwa na dhamira hiyo.
Chadema kimeeleza kuwa, taratibu za chama hicho kupata wagombea lazima zifuatwe, na kwamba Lissu ambaye ni mwanasheria mkuu wa chama hicho, kama yupo tayari kugombea nafasi hiyo, anakaribishwa.
“Akija na kuomba, atapewa,” amesema Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema na kuongeza “…kama tutakosa mtu aliyeomba, basi tutatafuta mtu ambaye hajaomba.”
Akizungumza na Nipashe hivi karibuni Dk. Mashinji amefafanua, kama Lissu atakuwa na dhamira ya kweli na kuchukua fomu, jina lake litapita katika mkondo ule ule kulingana na utaratibu wa chama hicho.
Akizungumzia utaratibu huo, kiongozi huo wa Chadema amesema, jina la Lissu litafikishwa katika sekretarieti ya chama hicho, na kwamba kama mengine yatakuwepo, yataingizwa kwenye hatua hiyo.
“Kamati Kuu hutoa idhini ya majina hayo kutangazwa, hivyo kutoa fursa ya kufanyiwa utafiti ili kupata jina moja litakalosimama kuwania urais,” amesema Dk. Mashinji.
Dk. Mashinji ametoa kauli hiyo huku mitandao ya kijamii ikihusisha safari za Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo za kumtembelea Lissu nchini Ubelgiji zikihusishwa na ushawishi wake kwa mwanasiasa huyo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki.
Ukaribu wa Lissu na Zitto unaonekana kuongezeka maradufu katika siku za hivi karibuni, jambo ambalo limezua sintofahamu kwa wawili hao.
Lissu anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji kutokana na kushambuliwa kwa risasi, miaka miwili iliyopita akiwa anatoka kuhudhuria kikao cha bunge mjini Dodoma, risasi 16 zilimpata.
Leave a comment