CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kitazindua rasmi mikutano ya hadhara kitaifa tarehe 21 Januari 2023, ikifuatiwa na uzinduzi wa mikutano hiyo katika ngazi ya Kanda nchi nzima. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, akitoa maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, iliyoketi jana tarehe 5 Januari 2023, kupokea na kujadili taarifa ya mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano baina yake na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kamati Kuu imetangaza kuwa uzinduzi rasmi wa mikutano ya hadhara kitaifa utafanyika tarehe 21 January 2023 na utafuatiwa na uzinduzi wa mikutano ya hadhara kila makao makuu ya Kanda na baadae ngazi nyingine za chama zitaendelea na mikutano kwenye ngazi zao,” imesema taarifa ya Mrema.
Katika hatua nyingine, Mrema amesema kamati hiyo imeagiza ngazi zote za Chadema kuendelea na maandalizi ya mikutano ya hadhara.
Aidha, Mrema amesema kamati hiyo imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano.
“Kamati Kuu imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano baina ya timu ya Chadema inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama, Freeman Mbowe na ile ya CCM/Serikali inayoongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana,” imesema taarifa ya Mrema.
Kamati Kuu ya Chadema imetoa maazimio hayo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuondoa zuio la mikutano ya hadhara, lililodumu Kwa takribani miaka sita tangu 2016.
Leave a comment