Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema kupangua wakurugenzi makao makuu
Habari za SiasaTangulizi

Chadema kupangua wakurugenzi makao makuu

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefanyia mabadiliko makubwa muundo wake wa sektarieti ya Kamati Kuu (CC), kwa lengo la kujipanga ili  kushika dola mwaka 2025. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, miongoni mwa mabadiliko hayo, ni kuziunganisha kwa baadhi ya kurugenzi zake zilizokuwapo, ili kuleta ufanisi na kufanikisha ushindi.

Kutokana na mabadiliko hayo, baadhi ya waliokuwa wakurugenzi, hasa wale ambao wameonakana kupwaya, wanaweza kujikuta moja kwa moja, wakitupwa nje ya ajira za makao makuu.

“Katika kikao chetu cha Zanzibar, tumejadili mengi, ikiwamo muundo wa kurugenzi zetu za makao makuu. Yote haya tunawekeza ili tuweze kuchukua dola mwaka 2025,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa kikao hicho, ambaye hakupenda kutajwa jina.

Amesema, katika mkutano huo wa siku takribani tatu, ambao ulilenga kuweka mkakati wa kuchukua madaraka ya kuongoza serikali kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama hicho kikuu cha upinzani nchini, “kimerudi kikiwa kimezaliwa upya.”

Viongozi wakuu wa Chadema, wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wajumbe karibu wote wa Kamati Kuu (CC), walijifungia Zanzibar, kupanga mikakati mahususi ya kisiasa kuelekea mwaka 2025.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Mtoa taarifa wetu anasema, pamoja na mengine, mikakati hiyo, ililenga kukisuka upya chama hicho, hasa katika kipindi hiki ambacho kiko nje ya Bunge.

Mbali na kujadiliana suala la kurugenzi za chama, kikao hicho maalum kilichopewa jina la “retreat,” kililenga kuweka mkakati wa kurejesha heshima ya chama hicho mbele ya wanachama na umma.

Mabadiliko ya muundo wa sektarieti, utakaokwenda sambamba na kuwafuta kazi baadhi ya wakurugenzi, unalenga  kukifanya chama hicho kuendelea kuongoza mapambano ya kudai haki.

Kwa sasa, Chadema inakabiliwa na hatari ya kuporwa usukani wa kuongoza upinzani nchini na chama cha ACT- Wazalendo, kufuatia Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa mmoja wa viongozi watatu wa juu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

Maalim Seif, ni Makamo wa Kwanza wa Rais Visiwani.

Miongoni mwa majukumu ambayo upinzani unakabiliana nayo, ni kuhakikisha kunakuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya, kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Chadema kilikwenda Zanzibar Jumanne iliyopita, “kuanza kikao maalum cha mkakati (retreat)” cha siku tatu, ambacho kililenga kupata mwelekeo wake mpya, unaotokana na wanachokiita, “figisu ilizokutana nazo katika uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba mwaka jana.”

Chadema kimejikuta kikianza upya safari yake ya kisiasa, kufuatia “kushindwa” vibaya kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Katika uchaguzi huo, chama hicho kiliambulia kiti kimoja cha ubunge wa majimbo kutoka wabunge wa 36 wa aina hiyo, waliopatikana mwaka 2015 na wabunge 19 wa viti maalum kutoka 35 waliopatikana mwaka 2015.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, Chadema kiliamua kutotambua matokeo mchakato wote wa uchaguzi na matokeo yake, ikiwamo kutotambua nafasi 19 za wabunge wake wa Viti Maalum.

Aidha, Chadema kilijadili hatima ya waliokuwa wanachama wake 19, waliofukuzwa uanachama, kutokana na utovu wa nidhamu, wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza lake la Wanawake (Bawacha), Halima Mdee.

Katika mkutano huo, wajumbe walikubaliana kuwa Mdee na genge lake, wamekiumiza sana chama hicho, baada ya kukubali kutumiwa na wanaokitakia mabaya na hivyo “matendo hayo maovu dhidi ya chama, hayana msamaha.”

“Pale Zanzibar, viongozi wameridhika kuwa Mdee na wenzake, wamekuwa wakitumika na CCM kwa maslahi binafsi na kwa malengo ya kuivurugu Chadema. Katika mazingira hayo, tumekubaliana kukitetea chama kwa gharama yoyote ile,” vimeeleza vyanzo vya taarifa.

Taarifa zinasema, wajumbe wa Kamati Kuu (CC), wamekubaliana kwenda mbele ya Baraza Kuu, ambako Mdee na wenzake wamewasilisha rufaa zao, ili kutetea maamuzi yake kwa maslahi ya chama na wananchi.

Anasema, “kama Mdee na wenzake wangekuwa wa kweli na kutaka suluhu, basi baada ya kukata rufaa zao Baraza Kuu, wangeacha kutumia jina la Chadema kujinufaisha binafsi na wangekacha mikutano ya Bunge hadi shauri lao limalizike.

“Lakini wameendelea kukichafua chama na kumdhihaki mwenyekiti wa chama. Hivyo basi, tumekubaliana kufika mwisho na watu hawa kwa kuachana nao moja kwa moja.”

Halima Mdee, Mbunge wa Chadema Viti Maalim

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa uanachama wa Chadema, 27 Novemba 2020, baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya utovu wa nidhamu, usaliti, kuhujumu chama, upendeleo, kutengeneza migogoro; na  kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama.

Mashitaka mengine, ni pamoja na kughushi nyaraka za chama na kwenda bungeni kujiapisha, kinyume na maekelezo na maamuzi ya chama chenyewe.

Wengine waliofukuzwa uanachama na Mdee, ni pamoja na waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti baraza hilo (Bara), Hawa Subira Mwaifunga.

Katika orodha hiyo, wapo pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi, Agnesta Lambat na naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Wengine, ni aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo; Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba,  Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana jijini Dar es Salaam, chini ya uenyekiti wa Mbowe, kilielezwa kuwa kitendo kilichofanywa na Mdee na wenzake, ni usaliti mkubwa na hivyo, adhabu pekee wanayostahili, ni kufukuzwa uanachama.

Ni kupitia mkutano huo, Mdee alitajwa kuwa ndiye kinara wa kundi hilo, lililopachikwa jina la Covid-19, katika mradi huo wa usaliti na kuhujumu chama, ambao uliratibiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wanachama wa CCM ambao awali walikuwa Chadema.

Aidha, Mdee anatuhumiwa kushirikiana na Tendega, Bulaya, Agnesta na Kunti, kupeleka majina Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Bunge, ili hatimaye wateuliwe na kuapishwa kuwa wabunge.

Vilevile, katika kutekeleza mradi huo, Mdee anaoenakana kuongea na baadhi ya viongozi wandamizi wa CCM, Bunge, NEC, pamoja na watu walioko “kwenye mfumo,” ili kufanikisha dhuluma dhidi ya wanawake wenzake wa Chadema.

Madai haya yanapata nguvu zaidi, kufuatia hatua ya serikali kumuachia huru Nusrat Hanje, kutoka gereza la Isanga, mkoani Dodoma, alikokuwa akishikiliwa kwa zaidi ya siku 140.

Nusrat, aliachiwa kutoka gerezani, usiku na siku ya tarehe 23 Novemba 2020 – siku moja kabla ya Mdee na kundi lake, kuapishwa na Spika Job Ndugai kuwa wabunge, katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.

Katika maelezo yake, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alisema, Nusrat na wenzake waliachiwa huru, baada ya Jamhuri kuona haina tena nia ya kuendelea na kesi.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Nusrat hakuwa miongoni mwa wanachama wa Chadema walioshiriki mchakato wa ndani wa chama hicho, katika kuwatafuta wabunge wake wa viti maalum.

Vilevile, Mdee na wenzake, wameapishwa kuwa wabunge, bila kujaza fomu Na. 8(d) wanayopaswa kujaza wabunge wa Viti Maalumu.

Kifungu C katika fomu hiyo, kinataka kuwapo uthibitisho wa vyama kutoka kwa katibu mkuu au naibu wake, pamoja na mhuri wa chama husika.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alinukuliwa akisema, “fomu Na.8(d) nilizoletewa na NEC bado ziko ofisini kwangu.”

Akaongeza, “NEC itueleze hawa imewateuaje bila kujaza hizi fomu ambazo bado ninazo?”

Mdee na wenzake 18, hawakujaza fomu hizo, hawakugonga mhuri, wala hawakwenda mahakamani kula kiapo, wakati hayo ni miongoni mwa masharti yanayopaswa kutekelezwa kwa mtu anayetaka kuwa mbunge.

Hatua ya Mdee kubeba baadhi ya maswahiba zake na kuwafanya wabunge, imewanyima fursa wanachama wa chama hicho wenye sifa zaidi ya kuwa wabunge.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!