July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema kumshughulikia mbunge wake wa jimbo

Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kwa tiketi ya Chadema

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitamshughulikia Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani, kutokana na uamuzi wake wa kwenda bungeni, kinyume na msimamo wake wa kususia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa jana Alhamis, tarehe 15 Julai 2021 na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, alipoulizwa kwa nini chama hicho hakijamchukulia hatua Aida, kama kilivyofanya kwa wabunge 19 wa viti maalumu, kwa kuwafukuza kwa kosa la usaliti.

Lissu aliulizwa swali hilo katika mjadala uliofanyika kwenye mtandao wa Club House, kuhusu uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kuitaka Chadema ieleze utaratibu iliyotumia kuwatimua wabunge hao 19.

Lissu amesema, Chadema hakijamuunganisha Aida katika sakata hilo lililomkumba Halima Mdee na wenzake 18, kwa kuwa suala lake liko tofauti.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema

“Sababu uwepo wake bungeni unatofautiana na wabunge 19, tunasema huyu tutamshughulikia kwa utaratibu wake wakati utakapowadia. Tutamuadhibu wakati muafaka wa kushughulika na Aida utakapofika,” amesema Lissu.

Aida aliingia bungeni baada ya kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mshindi wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ambayo Chadema iligoma kuyatambua.

Chadema iligoma kutambua matokeo ya uchaguzi huo, kwa madai kwamba mchakato wake haukuwa huru na wa haki. Hata hivyo, NEC imekanusha madai hayo ikisema, iliendesha uchaguzi huo kwa mujibu wa sheria.

“Aida alitangazwa kuwa mbunge wa Nkasi Kaskazini, kwa hiyo kesi yao iko tofauti na kesi ya Mdee na ndiyo maana hatuzungumzi sana,” amesema Lissu.

Makamu mwenyekiti huyo wa Chadema Bara, amesema chama hicho hakinufaiki na uwepo wa Aida bungeni.

“Aida sio kwamba tuna faidika na uwepo wake mule, kama tungekuwa tunafaidika na uwepo wake mule tungepokea ruzuku ya mbunge wa jimbo.”

“Kumbuka ruzuku ya vyama imegawanywa mafungu mawili, inayotokana na mbunge wa jimbo na kura za wabunge. Sisi hatupokei ruzuku yoyote, sio ya Aida au ile asilimia ya kura za wabunge. Hatufaidiki na uwepo wake,” amesema Lissu.

Mbali na Mdee, wengine waliotimuliwa Chadema ni, waliokuwa viongozi wa Bawacha, Hawa Mwaifunga (Makamu Mwenyekiti). Grace Tendega (Katibu Mkuu). Jesca Kishoa (Naibu Katibu Mkuu) na Agnesta Lambart (Katibu Mwenezi).

Wengine ni, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko, pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mtwara, Tunza Malapo.

Pamoja na Cecilia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropita Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Wanasiasa hao walifukuzwa Chadema tarehe 27 Novemba 2020, siku mbili baada ya kuapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwa wabunge viti maalumu pasina baraka ya uongozi wa chama hicho.

error: Content is protected !!