July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema kumburuza Magufuli Mahakamani

Msafara wa John Magufuli ukiwasili jijini Mwanza kwa ndege ya serikali

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kiko mbioni kufungua mashauri mawili mahakamani dhidi ya John Pombe Magufuli, mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mabere Marando, mwanasheria mkuu wa chama hicho, ameliambia MwanaHALISI Online, kesi dhidi ya Magufuli itafunguliwa mahakama kuu, haraka iwezekanavyo.

“Tutamshitaki Magufuli haraka iwezekanavyo. Huyu mtu ana sifa ya kutoheshimu utawala wa sheria, hivyo tunataka kumuonyesha kuwa nchi hii inatawaliwa kwa sheria,” anasema Marando kwa sauti ya ukali.

Anasema, chama chake kitafungua mashauri mawili Shauri la kwanza litahusu mwanasiasa huyo kuanza kampeni kabla ya wakati na jingine, ni juu ya matumizi ya vyombo vya serikali kwenye kampeni za kisiasa.

“Yote haya yatamhusu Magufuli na mawakala wake. Hatuwezi kuruhusu mtu mmoja au chama kimoja, kinatumia madaraka yake binafsi na sisi tunanyamaza,” ameeleza.

Marando anasema, katika shauri la kwanza, chama chake kitawaunganisha shirikisho la soka nchini (TFF); Baraza la Soka la Afrika Mashariki (CECAF); CCM na wakala wa ndege za serikali.

Anasema, TFF itaunganishwa katika shauri hilo kutokana na hatua yake ya kumualika Magufuli kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano yanayoandaliwa na CECAFA.

Hatua ya Chadema kuamua kufungua shauri dhidi ya mwanasiasa huyo imekuja baada ya Magufuli Dar kutumia ndege ya Serikali katika anachoita, “kampeni yake ya kichama ya kujitambulisha.” wakisema hatua hiyo ni matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa.

Magufuli, ametumia ndege ya serikali aina ya Fokker F28, alipokwenda Mwanza.

Lakini Nape Nnauye amesema, “…tumekodi ndege hii. Hatukupewa bure na yeyote anayetaka kuitumia aende kulipia tu, atapewa.”

Magufuli hakupatikana kueleza maoni yake juu ya hatua hiyo ya Chadema.

Katika hatua nyingine, Marando amesema, mbali na kufungulia mashitaka mahakamani dhidi ya Magufuli, CCM na mawakala wake, chama chake kitawasilisha pingamizi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuomba kumzuia Magufuli kuwa mgombea urais.

Anasema, “tutamuwekea pingamizi kwa kuanza kampeni kabla ya wakati. Tunataka tupate rais anayefuata sheria, siyo rais anayevunja sheria.”

error: Content is protected !!