May 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema kufunguka kuhusu Ben Saanane?

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kimekuwa kikilaumiwa kwa kukaa kimya tangu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa Bernard Saanane ambaye ni mtumishi makao makuu chama hicho kimeitisha mkutano na waandishi wa habari siku ya kesho, anaandika Charles William.

Chadema imekuwa ikipatwa na kigugumizi katika kutoa kauli ya kueleweka juu ya kutoweka kwa Ben ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti makao makuu ya wa chama hicho, huku suala hilo likizua hisia kuwa huenda chama hicho kinajua mahali alipo ndiyo maana kimeonesha ukimya.

Ben anadaiwa kutoweka tarehe 18 Novemba, 2016 na tangu siku hiyo mpaka leo ikiwa ni zaidi ya siku 26 kijana huyo hakuwahi kuonekana tena, kiasi cha kuzua hofu kubwa kwa ndugu, jamaa na marafiki huku familia yake ikimsaka kwa jitihada kubwa kiasi cha kutoa ripoti kwa Jeshi la Polisi.

Taarifa iliyotolewa leo na Tumaini Makene ambaye ni Ofisa Habari wa Chadema taifa imewaalika waandishi wa habari katika mkutano utakaofanyika makao makuu ya chama hicho siku ya kesho Jumatano.

“Tunaomba kukutaarifu na kualika chombo chako (mwandishi na mpiga picha) kwenye press conference itakayofanyika tarehe 14, Desemba, 2016 Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni kuanzia saa sita mchana,” imesema taarifa hiyo.

Ingawa taarifa hiyo haijaeleza kuhusu ajenda ya mkutano huo na wanahabari lakini ni wazi kuwa, suala la kutoweka kwa Ben halitaepukika kama si kuelezwa na Chadema basi kuhojiwa na wanahabari.

Hivi karibuni katika tamko lililotolewa na kundi la Umoja wa Kizazi Tanzania (UTG) chini ya mwenyekiti wake Godlisten Malisa pamoja na mambo mengine lakini pia walishangazwa na ukimya wa Chadema kuhusu kupotea kwa Ben ilihali alikuwa mtumishi wa makao makuu ya chama hicho.

UTG ambayo pia Ben ni katibu wake ilisema, “Hatujaridhishwa na namna Chadema inavyochukua hatua katika suala hili, Ben amekuwa mtumishi wa chama hicho kwa muda mrefu, hatuoni kama ni sahihi chama hicho kutotoa tamko lolote hadi leo ikiwa ni siku 24 tangu apotee.”

error: Content is protected !!